KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema kuwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ataapishwa rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Alhamisi ijayo Novemba 5, 2020.

Polepole amesema hayo leo Jumamosi, Oktoba 31, 2020, jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari na kuongeza kuwa ushindi uliyopatikana kwa CCM ni historia kubwa na heshima kwa chama hicho tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini.

“Tangu tukiengia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, haijawahi kutokea, CCM tumeshinda maradufu (zaidi ya asilimia 84) Urasi wa Tanzania na zaidi ya asilimia 76 nafasi ya urais Zanzibar, tumepata takribani viti vyote, ni heshima kubwa sana kwa chama chetu.

“Kesho Dkt. Magufuli atapokea hati ya ushindi kuwa ndiye Rais Mteule wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sherehe itakuwa ndogo tu ya takribani watu 400 kwa ajili ya kuwakilisha, huu si muda wa sherehe ni muda wa kufanya kazi.

“Novemba 5, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, kutakuwa na tukio kubwa la kuapishwa kwa Dkt. John Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mhula wake mwingine wa pili, karibuni mapema saa 12 asubuhi kushuhudia tukio hilo muhimu.


“Siku ya Jumatatu, Novemba 2, 2020, Dkt. Hussein Ally Hassan Mwinyi ataapishwa rasmi kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa awamu ya nane, wanachama wa CCM na wapenda demokrasia, sote tujitokeze kwa wingi katika hafla hiyo,” amesema Polepole.


 


 


“Leo hii kule ndege kubwa aina Dreamliner inaanza kutua Dodoma na Magufuli yupo kazini. CCM tuendelee kuchapa kazi kuliletea maendeleo Taifa letu, tuwalipe Watanzania uadilifu, unyenyeklevu na kuchapa kazi, hatutawaangusha Watanzania.


 


Aidha, Polepole amesema kuwa kuanzia leo, wabunge wateule, wawakilishi wateule na madiwani wateule wa CCM, wakati wakisubiri kuapishwa, waanze kuchambua ahadi zilizotolewa na wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar, wafuatilie kero na kuanza kazi mara moja. “Huu ni muda wa kufanya kazi na kuwatumikia Watanzania, hakuna sherehe,” amesema Polepole.


 


Akitangaza matokeo ya uvhaguzi Mkuu, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage alisema kuwa, Dkt. Magufuli ndiye mgombea aliyepata idadi kubwa zaidi ya kura 12,516,252 kati ya kura 15,091,950 zilizopigwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020, kuliko wagombea wengine 14 huku mpinzani wake mkuu, Tundu Lissu wa Chadema akiachwa mbali zaidi na kuwa wa pili kwa kupata jumla ya kura 1,933,271.