Rais Yoweri Museveni wa Uganda ashtumu vikali wanasiasa wanovunja masharti ya kudhibiti virusi vya corona wakati huu wa kampeni za uchaguzi wa rais.

Kauli hiyo imetolewa na mgombea huyo wa urais wa chama cha NRM, ikiwa leo ni siku ya tatu tangu mpinzani wake Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine alipokamatwa na jeshi la polisi kwa kufanya mkutano wa hadhara wa kampeni.

Rais Yoweri Museveni amesema hayo katika mkutano wa kampeni alipokutana na viongozi wa chama tawala mkoa wa Karamoja, Kaskazini Mashariki mwa Uganda wakati anatetea kiti chake cha urais kwa muhula wa sita.

‘’Tayari tumepoteza watu wengi wakiwemo wabunge wawili, tumepoteza wanasayansi hivyo ni uhalifu kwa mtu ambaye anavunja masharti. Kila mtu ni lazima afuate masharti yaliyowekwa na wizara ya afya’’, amesema Museveni.

Aidha, rais Museveni amesema wanasiasa hao wanaungwa mkono na watu kutoka nje wenye dhamira mbaya wasiopenda amani na utawala bora nchini Uganda.

Rais Museveni amesema hayo wakati mpinzani wake Bobi Wine, mgombea urais kupitia chama cha NUP akiwa amekamatwa polisi mjini Jinja kwa kosa la kukiuka masharti dhidi ya corona.

Kukamatwa kwa Bobi Wine kumesababisha zaidi ya mauaji ya raia 16 , majeruhi 60 na wengine 321 kushikiliwa na polisi wakati wa makabiliana na polisi wakitaka mgombea wao kuachiwa huru