Nyota wa muziki wa Hip Hop nchini, Hamis Mwinjuma @mwanafa amesema baada ya kupata nafasi ya Ubunge wa jimbo la Muheza juhudi zake anazihamishia kwa wananchi wa huko.


#MwanaFA alitangazwa kushinda kiti cha Ubunge kwa tiketi cha Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa jimbo hilo kwa kura 47,578 akifuatiwa na Yosepher Komba (Chadema) mwenye kura 12,034.


Kupitia mahojiano yake na Wasafi, #MwanaFA alisema kwa sasa muziki utasubiri kwanza kidogo ili afanye kazi ya wananchi kwa kujipanga kuwasemea wapiga kura wake na kutatua matatizo yao.


“Kitu ninachoangalia kwa sasa namna gani nitawatumikia wananchi wangu walioniamini na kunichagua. Nina deni kubwa kwao kuhakikisha nayabeba matatizo yao, kama muziki ni kitu ambacho hakichukui muda mrefu kurekodi naweza kufanya baadaye,” alisema.


Aliwashukuru wananchi wa huko kwa imani kubwa waliyomuonesha na kwamba anamuomba Mungu amsaidie aweze kutimiza kile alichokusudia.


Kuhusu wasanii wenzake wa vyama vya upinzani waliongushwa katika uchaguzi Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Joseph Haule ‘Professa Jay’ alisema anasikitishwa ila anawahimiza kuhamia kwenye chama chenye misimamo yake CCM kama itawapendeza.

“Natamani na wao wangekuwa ni wana Chama cha Mapinduzi tuwe pamoja. Ningependa wawe kwenye chama nilichopo, ni chama chenye msimamo wake,” alisema.