MWANZO zilikuwa ni tetesi tu kwamba, staa wa muziki barani Afrika na mmiliki wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ anammilikisha mali nyingi mama yake mzazi, Sanura Kassim ‘Mama Dangote’, lakini sasa kila kitu kimethibitika rasmi.
Awali ilielezwa kama tetesi kwamba, Diamond au Mondi amewanyima urithi wanawe aliozaa na wanawake watatu tofauti, lakini sasa siyo siri tena, kwani huo ndiyo ukweli wenyewe.
TETESI ZA AWALI
Wakati akinunua hoteli yenye hadhi ya nyota tatu maeneo ya Mikocheni jijini Dar, miezi kadhaa iliyopita, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilipokea habari nyeti kwamba, Mondi anammilikisha kila kitu mama yake huyo huku akiwa hataki kusikia suala la kuandika majina ya watoto wake katika miradi kibao anayoianzisha na mali anazonunua kama majumba ya kifahari, mashamba na mengineyo.
WATOTO WA MONDI
Gazeti la IJUMAA WIKIENDA linafahamu kwamba, Mondi amezaa watoto wanne na wanawake watatu tofauti ambao ni Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye amezaa naye watoto wawili, Latiffah Nasibu ‘Tiffah Dangote’ na Prince Nillan.
Wengine ni mwanamitindo Hamisa Mobeto ambaye amezaa naye mtoto mmoja, Dyllan na Tanasha Donna ambaye amezaa naye mtoto mmoja aitwaye Naseeb Junior. Uchunguzi wa Gazeti la IJUMAA WIKIENDA umebaini kwamba, hakuna mradi, kampuni wala mali yoyote ambayo imeandikwa jina la mtoto wake hata mmoja kati yao.
AVUNJA UKIMYA
Wakati jambo hilo likizungumzwa chini kwa chini na wanawake hao aliozaa nao wakiwa hawaamini, Mondi mwenyewe ameweka wazi kila kitu. Mondi anasema kuwa, hata ikitokea hayupo duniani, basi mama yake huyo ndiye atakuwa kila kitu na lazima apate haki yake.
Mondi anasema kuwa, mama yake ndiye msimamizi mkuu wa mali zake zote na ndiye amekuwa akimuandika jina lake kwenye miradi yake mbalimbali. Mondi ambaye anasifi ka kwa kuwa na mali nyingi kutokana na muziki wake, anasema watoto wake bado ni wadogo na yeye si mtu wa kujikweza kuanza kuzigawa mali kwa watoto.
“Mimi si mtu wa kujikweza kuonesha kwamba hii hoteli itakuwa ni ya Tiffah au Wasafi FM ni ya Nillan au Wasafi TV ni ya Dyllan.
“Watoto wangu bado ni wadogo sana, natamani wangekuwa wakubwa ili waweze kusimamia miradi yangu. “Natamani hata Tiffah angekuwa ananisaidia, lakini bado ni wadogo, si kwamba hawana haki, bali kila mtoto ana haki yake,” anasema Mondi.
MALI ZA MONDI
Baadhi ya mali anazomiliki Mondi ni pamoja na lebo ya muziki ya WCB, kituo cha runinga na redio cha Wasafi na kampuni nyingine mbalimbali. Hivi karibuni Mondi ametangaza kukamilika kwa jengo refu la Wasafi Tower jijini Dar huku akimiliki majumba ya kifahari ndani ya Bongo kama jijini Dar, mkoani Dodoma na kwingineko.
Pia anamiliki mjengo wa kifahari jijini Johannesburg nchini Afrika ya Kusini. Pia anamiliki magari ya kifahari kama Toyota Land Cruiser V8 na BMW X
TUJIKUMBUSHE
Miaka michache nyuma Mondi aliwahi kuposti katika ukurasa wake wa Instagram akimtakia heri ya kuzaliwa mama yake na kuandika ujumbe mzito uliosomeka kuwa nusu ya mali zake zitachukuliwa na mama yake huyo kwani alipitia magumu mengi wakati wa kumlea hivyo hakuna wa kumlinganisha naye.
“Ninasikitika wanapokuja na kujaribu kukulinganisha thamani yako kwangu na mtu yeyote na kusahau kuwa bila wewe kunizaa na kunilea kwa shida na taabu, leo hii hakuna yeyote angenijua au kuniona “Dharau na manyanyaso uliyopitia kwenye kunilea hakuna anayejua hadi leo waone nimekuwa mtu mbele za watu.
“Madale is your home (Madale ni nyumbani kwako) na ikitokea leo nimekufa pia nusu ya mali zangu ni zako,’’ aliandika Mondi na kusisitiza kuwa anapambana ili mama yake awe na furaha muda wote. Pia hivi karibuni amesema kuwa, amemnunulia mjengo wa kifahari ushuani Masaki jijini Dar ambako atamhamishia muda si mrefu.