LICHA ya kukubalika katika kazi yake nje na ndani ya Bara la Afrika, katika hali isiyokuwa ya kawaida, staa wa muziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amejikuta akishambuliwa na mawe na mashabiki waliotajwa kuwa na hasira kali, Gazeti la IJUMAA limeusoma mchezo kamili.


 


NI NCHINI MALAWI


Tukio hilo la Diamond au Mondi kushambuliwa kwa mawe limeelezwa kutokea nchini Malawi hivi karibuni wakati alipokuwa amekwenda kwenye ziara yake ya kimuziki.


 


Taarifa kutoka nchini humo zimeeleza kuwa, Mondi alipata dhahama hiyo baada ya kufanya shoo kwa muda mfupi tofauti na jinsi ilivyotarajiwa na ndipo mashabiki hao walipomvaa kwa kuhoji kuwa haiwezekani aimbe kwa muda mfupi.


 


“Haiwezekani watu tumelipa pesa zetu, halafu yeye anakuja anaimba kwa muda mfupi namna hii…hii ni dharau, kama amezoea kufanya hivi kwenye nchi nyingine, hawezi kutufanyia ujinga huu Malawi,” alinukuliwa mmoja wa mashabiki aliyehudhuria shoo hiyo.


 


FUJO KAMA LOTE


Kwenye video mbalimbali ambazo ziliambatanishwa na maelezo ya habari hiyo, walionekana vijana hao wenye hasira kali wakirusha mawe kumlenga Mondi aliyekuwa anashuka jukwaani, lakini bahati nzuri mawe hayo hayakumpata.


 


Jamaa huyo alionekana anainama, akaokota jiwe hilo kisha kulivurumisha katika eneo hilo alilokuwa Mondi, lakini hata hivyo jiwe hilo halikuleta madhara yoyote kwani licha ya kumkosa Mondi, lakini pia halikuwapata watu wengine waliokuwa karibu naye.


 


Mashabiki mbalimbali walionukuliwa na mitandao ya nchini humo, walisema Mondi aliwakwaza kwani ndiye msanii pekee ambaye walikwenda kumuona katika shoo hiyo, lakini akawa amewakatisha tamaa kwa kufanya shoo fupi.


 


“Pesa ni ngumu, mtu umejibana, ukaenda kununua tiketi, halafu mtu anakuja kufanya kitu cha hovyo namna hii kwa kweli siyo sawa,” alinukuliwa shabiki mmoja.


 


WALINZI WAMWOKOA KWA TABU


Kwenye vipande hivyo vya video ambavyo Gazeti la IJUMAA limevipata, walionekana walinzi walivyofanya kazi ya ziada kumuondoa Mondi kwenye eneo hilo bila kudhurika kwani jamaa walionekana wana hasira mno.


 


Lakini pamoja na kikundi hicho ambacho kilikuwa na hasira na kuonekana wakiropoka maneno makali kwa lugha ya Kabila la Chewa la nchini Malawi, mashabiki wengine walionekana kuwa wastaarabu na kuwasihi wenzao waache fujo.


 


Mashabiki waliokuwa wakituliza fujo hizo, kwa upande wao walionekana kuridhika na kile kilichofanywa na Mondi alipokuwa jukwaani na kwamba muda haukuwa mchache kama watu hao walivyokuwa wanavyosema.


 


MONDI AWASHUKURU


Pamoja na kukutana na kisanga hicho, kwa upande wake, Mondi, kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 11, aliweka kipande cha video ya shoo yake hiyo ya na kuwashukuru kwa upendo mkubwa waliouonesha kwake.


 


Mondi hakuwa na kinyongo na kikundi hicho cha watu na badala yake alikijibu kwa kuwaonesha ni jinsi gani kulikuwa na ‘vaibu’ kama lote kwa wakati ambao alikuwa akifanya makamuzi jukwaani.


 


Kwenye moja ya vipande vya video alivyoviweka Mondi kwenye ukurasa wake, meneja wake wa shoo za kimataifa, Sallam SK alichagiza hoja hiyo kwa kukomenti kuwa, shoo hiyo ilikuwa nzuri na kumtaka Mondi aweke video nyingine.


 


“Eti wenyewe wamejitengenezea stori sijui chupa sijui, mawe ilimradi wapate followers, hebu posti clip zote tujionee chupa siye…” Aliandika Sallam.


 


Mondi amekuwa akifanya shoo nyingi kwenye maeneo tofauti ndani na nje ya Afrika ambazo zimekuwa zikijaza na kwenye shoo hizo, ni nadra mno kusikia amefanyiwa tukio kama hilo lililodaiwa kutokea Malawi.