Majeshi ya Misri yametoa taarifa kuhusu mpango wa kufanyika  mazoezi ya pamoja ya anga ya kijeshi kati ya nchi hiyo na Sudan katika anga ya Sudan.

Gazeti la al Ahram la Misri limenukuu taarifa ya majeshi ya nchi hiyo ikisema kwamba askari wa jeshi la anga la Misri jana Jumamosi waliwasili katika kituo cha kijeshi cha Meroƫ nchini Sudan kwa ajili ya mazoezi hayo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo,  mazoezi hayo ya kijeshi yamepewa jina la "Tai wa Mto Nile 1" na yatafanyika kwa kushirikiana na jeshi la anga la Sudan. Mazoezi hayo yataendelea hadi tarehe 26 mwezi huu wa Novemba.

Mazoezi ya kijeshi baina ya vikosi vya anga vya Sudan na Misri yanafanyika huku kukiwa na mzozo baina yao na nchi jirani ya Ethiopita kuhusu ujenzi wa bwawa la al Nahdha nchini Ethiopia. Wachambuzi wanasema, huo ni ujumbe maalumu wa Cairo na Khartoum na serikali ya Addis Ababa.

Karibu mwaka mzima sasa nchi hizo tatu zina mzozo kuhusu bwawa hilo. Mzozo huo umekuwa mkubwa kiasi cha kupiga kengele ya hatari na kuongeza uwezekano wa kushambuliwa kijeshi bwawa hilo. Serikali ya Ethiopia imepiga marufuku ndege kuruka katika anga ya eneo la bwawa hilo na imeongeza ulinzi ikisisitiza kuwa imejiandaa kwa hali yoyote ile.

Mazungumzo baina ya nchi hizo tatu yameshafanyika mara chungu nzima bila ya mafanikio. Misri inadai kuwa bwawa la al Nahdha litapunguza kiwango cha maji ya Mto Nile yanayoelekea Misri, wakati Ethiopia inajitetea kwa kusema, ina haki ya kutumia rasilimali za nchi yake kuwaletea watu wake maendeleo na ustawi.