WAKATI Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeanza kikao chake cha dharura, jijini Dar es Salaam, kujadili tuhuma za usaliti zinazowakabili wanachama wake 19, wakiongozwa na Halima James Mdee, inasemekana wanachama hao wako mbioni kufungua kesi mahakamani, kupinga kujadiliwa na chama chao.

 

Kwa mujibu wa taarifa zinazonukuu vyanzo mbalimbali, kesi hiyo, inatarajiwa kufunguliwa Jumatatu ijayo katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma

 

Mdee ambaye ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), anatuhumiwa kwa makosa matano, likiwamo kukaidi maelekezo halali ya chama chake, usaliti, utovu wa nidhamu na kushirikiana na maadui wa chama hicho.

 

Mkutano huo wa siku moja, unaongozwa na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Freeman Mbowe, na unafanyika katika hoteli ya Bahari Beach, jijini Dar es Salaam.

 

Wengine wanaoshitakiwa pamoja na Mdee, ni Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace Tendega; Makamu Mwenyekiti, Hawa Mwaifunga; Katibu Mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC), Ester Bulaya.

 

Wanachama wengine wanaokabiliwa na tuhuma hizo, ni Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Serengeti, Esther Matiko; Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

 

Katika orodha hiyo, wapo pia aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum, mkoani Arusha, Cecilia Pareso; Sophia Mwakagenda, Naghenjwa Kaboyoka, Kunti Majala, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Lwamlaza, Stella Siyao, Asia Mwadin Mohamed na Felister Njau.

 

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao hicho kilichoanza kilichoanza asubuhi ya leo Ijumaa, tarehe 27 Novemba 2020, watuhumiwa wote 19, wamegoma kuhudhuria mkutano huo.

 

Aidha, hadi saa 7 na dakika 40 mchana, wakati wajumbe wa Kamati Kuu walipotoka kwa ajili ya chakula, siyo Mdee wala wenzake hao 18, ambao wengine ni wajumbe wa kamati kuu, walionekana kwenye eneo hilo.

 

Badala yake, taarifa zinanukuu vyanzo vya habari kutoka kwa baadhi ya watu walio karibu na wabunge hao zikisema, watuhumiwa hao hawakufika kwenye kikao hicho, kwa kuwa wako mbioni kufungua kesi mahakamani, kupinga kujadiliwa na chama chao.

 

Kesi hiyo, inatarajiwa kufunguliwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Jumatatu wiki ijayo. Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene amesema, mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Mbowe ataongea na waandishi wa habari. Hata hivyo, Makene hajaeleza wazi kwa nini Mdee na wenzake hawajafika mbele ya kamati hiyo.