Makatibu Wakuu SADC -TROIKA wajadili hali ya siasa, ulinzi na usalama
Na Mwandishi wetu, Gaborone
Makatibu Wakuu wa SADC -TROIKA wamekutana na kujadiliana Mambo mbalimbali yakiwemo masala ya hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ndani ya SADC mjini Gaborone, Botswana.
Awali, Mkutano wa Makatibu Wakuu ulifunguliwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana, Bw. Gaeimelwe Goitsemang ambae pia alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo.
Ni mara ya kwanza kwa Kamati ya Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC) kukutana ana kwa ana tangu ulipotokea ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (Covid-19).
Kwa upande wa Makatibu wakuu waliohudhuria katika Mkutano huo kutoka Tanzania ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe.
Mkutano wa Makatibu Wakuu utafuatiwa na Mkutano wa Dharua wa Baraza la Mawaziri wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano katika Siasa, Ulinzi na Usalama baadae leo mchana mjini Gaborone.