RAIS John  Magufuli amesema kazi ya kuteua mawaziri ni ngumu, hivyo lazima amtangulize Mungu, ili anayestahili asije akamuonea, huku akiongeza kuwa mwaka huu atachelewa kuchagua Baraza la Mawaziri ikilinganishwa na Mwaka 2015 kwani wakati huo ilikuwa rahisi kwa sababu wabunge wa CCM walikuwa wachache.

Magufuli amesema hayo leo Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, leo Jumatatu, Novemba 16, 2020, wakati akimuapisha Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, na kusema kuwa kuendelea kwake kukaa madarakani kutategemea na utendaji wake kwa kipindi cha pili cha serikali ya awamu ya tano, na kuongeza kuwa lazima apitie kwa kina sifa na wasifu wa wabunge watakaopendekezwa katika baraza la Mawaziri ili aunde Baraza litakalomsaidia kuiletea maendeleo Tanzania.

“Nawapongeza walioapa leo, Mawaziri wawili na Waziri Mkuu, ni lazima nikiri kwamba sikuwa na haraka sana ya kuteua Baraza la Mawaziri, tuna Wabunge zaidi ya 350, na bado kuna nafasi 10 za Mimi kuteua, nafasi za Mawaziri na Manaibu Waziri haziwezi kufika 30, hata ungekuwa wewe unateua ungepata shida kubwa.

“Kwa kuwa nitachelewa kidogo, inaweza kuchukua hata miezi mitatu, kuunda Baraza la Mawaziri nikasema tuwe na Waziri wa Fedha na kwenye Mambo ya Nje nikaona hatuwezi kosa mtu wa kutusemea watu wakawa wanatutukana tukakosa majibu nikaona huyu Kabudi kwa kuwa alimudu nafasi yake acha aendelee.

“Lazima ni-check jina kwa jina na factors nyingi nyingine unazitafuta umtoe kwa sababu huwezi kwenye mkoa mmoja ukawa na wabunge hata watano lazima kuwe na division huo ndiyo ukweli, lazima uwe fair na umtangulize Mungu kwamba anayestahili usije ukamuonea. Wabunge presha mzishushe, kazi mliyoomba ni Ubunge sio Uwaziri, ningewaomba wabunge presha tuzishushe kwa sababu kazi tulizoomba ni ubunge na siyo uwaziri.

“Wizara nyingine zinasimama ili nijiridhishe, siteui mapema, Makatibu Wakuu wapo wafanye kazi zao, najua maneno ni mengi, Wabunge mnaotaka Uwaziri kwa Waganga nendeni tu shauri yenu, wengine watawapaka mikosi..ila najua hamuendi mnaenda kumuomba Mungu.

“Mawaziri wawili niliowateua sio kwamba ni maarufu sana kuliko waliobaki, nimeona kwa sababu nitachelewa kidogo kuwa na Baraza la Mawaziri na Wabunge lazima mlipwe posho na mishahara nikasema lazima tuwe na Waziri wa Fedha maana hatuwezi kusubiri miezi yote mitatu au minne.


“Washauri wangu wameniletea ushauri kwamba Wizara ya Ulinzi na Mambo ya Ndani ungeteua Mawaziri pia, wala sikuwajibu, sio lazima uwe na Waziri wa Ulinzi, CDF akitaka kupigana haendi kwa Waziri anaenda kwa Rais ndie Kamanda Mkuu, Polisi wakitaka kufanya kazi yao IGP anatosha.