KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, shabiki wa Simba ambaye pia ni mwanachama wa timu hiyo kutoka wilayani Misungwi jijini Mwanza, alifariki dunia juzi wakati mchezo wa Yanga na Simba ukiendelea.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1 huku bao la kuongoza la Yanga likipatikana kwa penalti iliyodaiwa kuwa tata baada ya Joash Onyango kumchezea madhambi Tuisila Kisinda dakika ya 30 na mwamuzi akatafsiri kwamba ilikuwa ndani ya eneo la hatari wakati mashabiki wengi wanadhani ilikuwa ni nje kidogo ya eneo hilo.Katibu Mkuu wa Matawi ya Simba Mkoa wa Mwanza, Philbert Kabago, ameliambia Championi Jumatatu kuwa ni kweli shabiki huyo alifariki dunia wakati mchezo ukiendelea.


 “Kweli mwanachama mwenzetu wa Simba aliyejulikana kwa jina la Shaban Balwe, alifariki dunia juzi Jumamosi wakati mchezo wetu na Yanga ukiendelea, kiukweli ni taarifa ambazo zilitushtua lakini ndio kazi ya Mungu, haina makosa.


“Tukio zima lilikuwa hivi baada ya mchezo kufika dakika ya 31 na Yanga kupata penalti iliyopigwa na Michael Sarpong, mwenzetu Shaban alipata mshtuko wa moyo baada ya kutokea kwa penati ile. Baada ya kupata mshtuko hali yake iliendelea kuwa mbaya na hata jitihada za kumpeleka hospitali zilipofanyika alifariki wakati akielekea hospitali kupatiwa matibabu, kiukweli imetuuma lakini hatuna jinsi,” alisema katibu huyo.


Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Misungwi (OCD), Benevenuto Shabu, simu yake haikupokelewa wala hakujibu meseji ambazo aliandikiwa na gazeti hili jana mchana.