Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara maarufu, Tariq Machibya(29) maarufu Mr. Kuku, imeahirishwa hadi Novemba 16, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutokana na upelelezi kutokamilika.

Wakili wa serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, ameileza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamailika.


Katika hati ya mashtaka mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 60/2020, miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya  kusimamia na kuendesha biashara ya haramu ya upatu, kupokea maingizo ya fedha kutoka kwa umma bila kuwa na leseni na kutakatisha fedha.


Inadaiwa kuwa kati ya Januari 2018 na Mei 2020, katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa anadaiwa kusimamia biashara ya upatu.


Pia Machibya anadaiwa alijihusisha na biashara ya upatu kwa kukubali na kukusanya fedha kutoka kwa umma, akijifanya kwamba watafanya ujasiriamali wa ufugaji wa kuku na wangepata faida ya asilimia 70 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa miezi minne na asilimia 90 ya mtaji wa awali waliowekeza kwa kipindi cha miezi sita, kiasi ambacho ni kikubwa katika biashara kuliko mtaji uliokusanywa.


Inadaiwa  kati ya April 26, 2019 na Januari 26, 2020 maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, alijihusisha na miamala ya Shilingi bilioni  6.4 kwa kutoa fedha hizo kutoka katika akaunti inayosomeka kwa jina la Mr Kuku Farmers Ltd, iliyopo katika benki ya CRDB, wakati akijua kuwa fedha hizo ni zao tangulizi la biashara haramu ya upatu.


Pia anadaiwa kupokea fedha za maingizo ya umma kiasi cha Shilingi bilioni 17 bila kuwa na leseni.