Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amerefusha muda kutotembea usiku nchini humo hadi Januari 3, kama sehemu ya hatua za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona, baada ya idadi ya maambukizi kuongezeka mwezi Oktoba. 


Kenyatta amesema mwezi huo pekee wa Oktoba, idadi ya maambukizi mapya ilipanda kwa 15,000, na taifa hilo liliripoti vifo karibu 300. 


Serikali iliruhusu baa kufunguliwa tena Septemba 28, na kupunguza muda wa kutotembea usiku kwa saa mawili, huku shule zikifunguliwa kwa sehemu Oktoba 12. 


Kenyatta amesema pia anasitisha mikutano yote ya kisiasa kwa siku 60, na amewaomba maafisa waandamizi serikalini kufanya kazi kwa njia ya mtandao. 


Wizara ya afya nchini humo imeelezea wasiwasi kwamba kurejea kwa mikutano ya kisiasa mwanzoni mwa Oktoba kunaweza kuwa miongoni mwa sababu za kusambaa kwa virusi hivyo.