CEDRIC Kaze, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa uwezo wa kiungo wake raia wa Angola Carlos Carlinhos ni wa hali ya juu jambo ambalo litampa upana wa kupanga kikosi namna atakavyohitaji.


Kwa sasa Yanga ipo kwenye maandalizi ya mchezo wake dhidi ya Namungo FC unaotarajiwa kuchezwa Novemba 22, Uwanja wa Mkapa saa 1:00 usiku.


Muangola huyo ndani ya Yanga amehusika kwenye mabao matatu kati ya 12 akifunga bao moja Oktoba 3 wakati Yanga ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union na alitoa pasi mbili za mabao.


Akizungumza na Saleh Jembe, Kaze amesema kuwa wachezaji wake wote ni muhimu ndani ya kikosi jambo hilo linamfanya aweze kuwa na chaguo namna atakavyosaka ushindi kutokana na kurejea kwa Carlinhos.


"Ninaona kwamba wachezaji wote wapo vizuri ila kurejea kwa Carlinhos kutaongeza chaguo katika kupanga kikosi.


"Bado tuna kazi kubwa ya kufanya na nina amini kwamba tutaendelea kupata matokeo mazuri ndani ya uwanja kwa kuwa wachezaji wapo tayari hivyo mashabiki watupe sapoti," amesema.


Yanga ipo nafasi ya pili kwenye  msimamo ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi 10. Nyota huyo alikuwa nje kwa muda kutokana majeraha ya enka ila kwa sasa amesharejea uwanjani.