Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe amesema wanachama wa CHADEMA walioenda Dodoma kuapa Novemba 24 kama Wabunge wa Viti Maalum wamevuliwa nyadhifa zao zote ndani ya chama hicho.


Pamoja na kuvuliwa nyadhifa zao uanachama wao unakoma tangu leo. Amesema hayo ndiyo yaliyoazimiwa na Kamati Kuu ambayo iliwaita kuongea nao ila hakutokea.

Mbowe anasema viongozi hao walikuwa wanasema wanahofia usalama wao kwenda Makao Makuu na waliamua kwenda katika eneo salama ili wazungumze nao lakini Wabunge hao hawakwenda.

“Kama vyama vya siasa tunakwazwa sana kuona Dada zetu, Viongozi wenzetu, mama zetu na wengi wao walikuwa wagombea wa ubunge walionyang’anywa ushindi mchana kweupe wanakwenda kuapa kwa Spika Ndugai”

Amesema,”Wanaapa wakati Majimboni kwao wameacha Wanachama wetu, Wapiga kura wao wanasota kwenye Magereza. Nchi nzima leo tuna kesi zaidi ya 450 za Wanachama wetu ambao wameshtakiwa kwa makosa ya kihuni ya ajabu”