Wakati mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwa ‘imechafuka’ kwa picha za magari na mijengo ya kifahari ya mfanyabiashara maarufu katika ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika, Genius Kadungure ‘Ginimbi’, imeelezwa kuwa roho ya kijana huyo imetwaliwa na jumuiya ya siri ya Freemason, Gazeti la IJUMAA Wikienda lina kisa na mkasa wa kutisha.

Ginimbi (36) ambaye pia alikuwa ni shemeji yake mzazi mwenza wa msanii maarufu nchini, Nasibu Abdul ‘Diamond’; Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’, alipoteza maisha Novemba 8, mwaka huu katika ajali ya gari.

Ajali hiyo ilitokea wakati akirejea kutoka kwenye sherehe kuzaliwa ‘birthday party’ ya mchepuko wake aliyefahamika kwa jina la Michelle Amuli maarufu Mimi Moana (26). Ndani ya gari lake la kifahari aina ya Rolls Royce Wraith alilokuwa akiendesha, mbali na Ginimbi na mwanadada Moana, walikuwepo watu wengine wawili ambao wote kwa pamoja walipoteza maisha.

Kwa mujibu wa Gazeti la iHarare, watu hao wengine wawili ni Limumba Karim ambaye ni raia wa Malawi aliyekuwa akitafutwa kwa tuhuma za utapeli na mwanamke mmoja, raia wa Msumbiji aliyetambulika kwa jina la Alichia Adams.

Inaelezwa kuwa Ginimbi alikuwa anaendesha gari hilo kwa kasi, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na gari lingine ina ya Honda kisha kupoteza mwelekeo na kuparamia mti. Gari hilo liliwaka moto uliowaunguza pakubwa watu wanne waliokuwa ndani yake.

Polisi wa Zimbabwe walithibitisha kuwa watu watatu walifariki dunia papo hapo baada ya kuungua, lakini Ginimbi alifariki dunia dakika tano baada ya kutolewa ndani ya gari hilo.

FREEMASON WATAJWA


Wakati Wazimbabwe wakiendelea kujazana barabara kumuaga na kuomboleza kifo cha bilionea huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa zaidi ya shilingi bilioni 200, baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa kifo chake kimesababishwa na Freemason baada ya kukiuka masharti.


Freemason ambayo ni jumuiya ya siri inayodaiwa kutoamini uwepo wa Mungu, wamedaiwa kuwa chanzo cha utajiri wa Ginimbi ambaye alikuwa anamiliki magari mbalimbali ya thamani ya zaidi ya Sh bilioni 3.1.


Kwa mujibu wa mwandishi wa habari kutoka Nigeria, Kemi Olunloyo, Ginimbi alipanga kifo chake baada ya kubaini kuwa amekiuka masharti kwa kufichua baadhi ya siri zake.


“Video aliyoitupia mitandaoni muda mchache kabla ya kuelekea kwenye birthday, alionekana kuwa na furaha na aliwaambia watu nini kinakwenda kutokea.

“Lakini pia alikuwa na jeneza ndani ya chumba chake, haya yote watu walikuwa hawaelewi kuwa ni mojawapo ya taratibu za kifreemason,” anasema.


Hoja hiyo ilikuwa mkono na nabii wa kike, mwandishi wa vitabu na mmiliki wa tovuti, Mary-Tamar ambaye ni maarufu kwa jina la Jean Gasho ambaye alisema mwezi Novemba, ni mwezi maalum wa kutoa kafara. Nabii huyo ambaye pia ni raia wa Zimbabwe alisema Wazimbabwe wengi hutoa kafara katika mwezi Novemba na hakuna anayeweza kuelezea sababu za kuuchagua mwezi huo.


“Vivyo hivyo kwa Ginimbi, kwa maono yangu kama nabii niliona kifo chake, alikuwa ni mmoja wa watu walionitesa katika kuwaombea hasa ikizingatiwa alikuwa amejiunga na jumuiya hiyo isiyoamini uwepo wa Mungu.


“Hakika mwisho wake, umekuwa sadaka kwa miungu yake ambayo ndiyo iliyompatia utajiri wa kutisha,” anasema.


Mbali na hao, pia mchungaji kanisa moja jijini Harare ambaye pia ni wakili, Joshua Zim naye alidai kutabiri kifo cha Ginimbi saa 72 kabla ya tukio hilo la ajali. Mchungaji huyo alidai kuwa aliwaambia Wazimbabwe wamuombee Ginimbi kwa kuwa alikuwa amepata maono ya jambo baya liloweza kumtokea.


ZARI AMLILIA

Awali, Zari aliposti kwenye akaunti yake ya Instagram kuelezea mshtuko na masikitiko kuhusu kifo hicho. Hata hivyo, Zari ambaye anadaiwa kuelekea nchini humo kuhudhuria mazishi ya bilionea huyo, alikuwa rafiki wa karibu wa aliyekuwa mke wa Ginimbi, Zodwa Mkandla.


ALINUNUA JENEZA LAKE


Aidha, katika hali ya kushangaza taarifa zinaeleza kuwa wiki moja kabla ya kifo, Ginimbi alinunua jeneza lake lenye thamani kubwa kwa ajili ya kutumika siku atakapotoweka duniani.


Jeneza hilo limeelezwa kukutwa ndani ya chumba cha Ginimbi, jambo ambalo liliwafanya watu wabaki midomo wazi. Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), Ginimbi na mpenzi wake, Moanna wanadaiwa kuona viashiria vya mwisho wao.


Katika posti yake ya mwisho, Ginimbi aliposti video kwenye akaunti yake ya Instagram ikimuonesha akiingia kwenye gari lake kwenda kusherehekea birthday hiyo katika klabu maarufu ya usiku ‘Dreams Night Club’ ambayo anaimiliki. Katika video hiyo alisema; “Tunakwenda kufungua shampeni, unakwenda kuwa usiku wa kuogelea shampeni.”


SAFARI YA UTAJIRI

Wakati mazishi yake yakiendelea kuwa gumzo, upande wa pili utajiri wake pia nao umezidi kuwaweka watu njia panda kutokana na magari ya kifahari na majumba aliyokuwa anayamiliki kijana huyo. Ginimbi, safari yake kimaisha aliianza mwaka 2000 kwa kujishughulisha na uuzaji wa mitungi ya gesi.

Wakati huo akiwa na umri wa miaka 17 anaidawa kuifanya biashara hiyo ambayo ilimpatia uzoefu mkubwa uliomkutanisha na rafiki yake aliyekuwa anafanya kazi katika ofisi za Shirika la Ndege la Angola.


Kwa mujibu wa taarifa zake, hapo ndipo siri ilipojificha kwani tangu alipokutana na rafiki yake huyo, inaelezwa mambo yalimnyookea Ginimbi ambaye alianzisha kampuni yake ya kusambaza gesi ijulikanayo kama Pioneer Gases.


Kampuni hiyo ambayo sasa ni kubwa katika ukanda huo ina matawi nchi za Zimbabwe, Botswana na Afrika Kusini. Ndani ya miaka miwili alipata magari mawili likiwemo Mercedes Benz S class.


Ginimbi alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Piko Trading ambayo inamiliki Makampuni ya Rivonia Gases, City Centre Freight, Pioneer Gases and Quick Gases ambazo zote ofisi zake zipo katika nchi za Zimbabwe, Afrika Kusini na Botswana.


Aidha, mkewe aliyefahamika kwa jina la Zodwa Mkandila ambaye wana watoto wawili, pia ni mfanyabiashara mkubwa Zimbabwe. Anamiliki Kampuni ya Traverze Travel ambayo alianzisha mwaka 2003 baada ya kuacha kazi ya mapokezi ‘receptionist’ katika ofisi moja.

ANAVYOMILIKI NI BALAA

Ginimbi anamiliki majumba ya kifahari yaliyopo majiji ya Harare, Johanessburg na Gabarone. Pia anamiliki magari ya kifahari aina mbalimbali kama RR, Autobiograph Range, Bentely, Lamborghini na Ferrari, yote yanakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.1.

Wakati wengi wakitilia shaka utajiri wake, Oktoba 3, mwaka huu aliongeza gari la kifahari aina ya Lamborghini lenye thamani ya Dola za Kimarekani 600,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.3 za Kitanzania).

Gari lake hilo la kifahari lilizua gumzo kwa watu wengi katika Mji Mkuu wa Zimbabwe, Harare. MISUKOSUKO Mei 2014, Ginimbi alikamatwa kwa madai ya utapeli zaidi ya Sh. milioni 200.

Alituhumiwa kumtapeli mbunge wa chama tawala nchini Zimbabwe (ZanuPF), Chegutu Magharibi Dexter Nduna. Nduna ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Badon Enterprises na mchimba madini ambaye pia ni maarufu nchini humo kwa jina la Gatawa.


Ginimbi alituhumiwa kusajili kampuni ya uongo inayoitwa Transco Civil Engineering huko Afrika Kusini na kufungua akaunti ya katika benki moja. Kisha aliwasiliana na mbunge huyo kwa njia ya simu kuwa yeye ni mkurugenzi wa kampuni hiyo na kwamba anatafuta soko la pampu zinazotumika katika uchimbaji wa madini.

Gatawa alidaiwa kumtuma kaka yake, Enock kwenda Afrika Kusini kununua pampu hizo. Ginimbi alidaiwa kumwelekeza Enock kuweka kwenye akaunti ya benki ya kampuni kiasi cha fedha zaidi ya shilingi milioni 300 kwa ajili ya kununua pampu hizo 10.

Baada ya uhamisho huo wa pesa, Enock aliambiwa na maofisa wa kampuni ya Ginimbi, Transco Civil Engineering arejee Zimbabwe na kusubiri kifurushi chake baada ya siku tatu. Hata hivyo, ilielezwa kuwa baada ya muda huo alipokea kifurushi kilichojazwa chaja za smartphones.

Misukosuko mingine ikiwemo utakatishaji pesa pamoja na ukwepaji wa kodi pindi alipokuwa ananunua magari yake. Ginimbi alidaiwa kukwepa kulipa ushuru hatua ambayo ilimsababishia kukutana na makucha ya Mamlaka ya Mapato Zimbabwe (Zimra) wakati aliponunua gari aina ya Bentley Continental GT.

MAZISHI YAKE

Aidha, katika mazishi yake yanadaiwa kuwa yamefanyika Novemba 14, mwaka huu, Jeshi la Polisi nchini humo lilizuia mamia ya watu kuhudhuria mazishi yake na kuagiza idadi isyozidi 100 ili kuzuia maambukizi ya Corona.


 


Msemaji wa Polisi nchini humo, Paul Nyathi alisema kwa kuwa Corona imeshachukua maisha ya watu zaidi ya 255, ni lazima raia wa nchi hiyo kuheshimu maagizo ya Polisi.

Awali polisi pia walizuia sherehe ya kumuaga iliyotakiwa kufanyika Novemba 13, mwaka huu, lakini pia likazuia sherehe yoyote ikiwemo wasanii kupafomu katika mazishi yake.

Hata hivyo, msemaji wa familia, Clement Kadungure alikanusha kuwepo kwa mashrti ya kuhudhuria mazishi yake kama vile kuvaa nguo nyeupe na kwenda na kinywa chako (kilevi). Kadungure alisema mazishi yake yanafanyika kwa kuzingatia taratibu zote za tamaduni za Zimbabwe ikiwemo ibada maalum ya kumuaga.

Pia alikanusha taarifa za Ginimbi kuzikwa ndani ya jumba lake la kifahari na badala yake alidai kuwa atazikwa katika makazi yake yaliyopo huko kijijini kwake, Domboshava -Zimbabwe.

Hata hivyo, hakukanusha taarifa za bilionea huyo kuzikwa na gunia lilojaa Dola za Kimarekani. Kwa mujibu wa Gazeti la Herald, mfanyabiashara huyo aliyeishi maisha ya kifahari aliacha maagizo hayo kwa wanachama wa All-White Funeral.

Stori: Harare, Zimbabwe