Jonas Kamaleki,MAELEZO
Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kwa kuwa na rasilimali nyingi zinazoweza kuifanya nchi hii kujitegemea kiuchumi hadi kuzifadhili nchi nyingine duniani endapo zitaendelea kusimamiwa vizuri.


Licha ya kuwa na madini ya Tanzanite ambayo hupatikana nchini tu katika dunia, ipo pia gesi ya Helium ambayo inapatikana kwa futi za ujazo bilioni 138.


Kiwango hiki ni kikubwa kiasi kwamba Tanzania inaweza kuuza gesi hiyo kutosheleza mahitaji ya dunia nzima. Kwa sasa Marekani ndiyo inaongoza kwa kusambaza Helium kwa aslimia 50.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ernest Mulaya akihojiwa hivi karibuni na TBC1 anasema kuwa kwa idadi ya watu wote duniani zaidi ya bilioni 7, gesi ya Helium iliyopo Tanzania kila mtu anaweza kugawiwa lita 500 za gesi hiyo.


Huu ni utajiri mkubwa ambao ukitumiwa vizuri nchi hii uchumi wake utapanda kwa haraka na kufanya maisha ya watanzania kuwa bora zaidi.


Akizindua Bunge la 12 jijini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alisema, “Tuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo zinaweza kuhudumia dunia kwa miaka 20. Hii ndiyo sababu, kila siku nimekuwa nikisema, sisi sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni tajiri sana.”


Gesi ya Helium inayopatikana  mkoani Rukwa inatajwa kama hazina kubwa zaidi duniani inategemewa kuziba pengo la upungufu wa helium lililopo duniani kwa sababu matumizi na mahitaji yake yameongezeka katika teknolojia mbalimbali za kimkakati.


Helium hutumika katika teknolojia ya kutengeneza vifaa vya maabara, roketi kupozea aina za sumaku, mitambo ya kinyuklia, vifaa vya elektroniki vingi na vinavyotumika katika maisha ya kila siku kama mashine za kudurufu na zile za afya kama CT –Scan na MRI. 


Mwisho