TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, imemtaka Mkurugenzi wa kampuni ya Farm Green Implement (T) Ltd, Dunga Othman Omar kurudisha shilingi milioni 33.2 za wakulima wawili wa Wilayani Hanang' alizochukua ili awanunulie matrekta mawili.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati jana, Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara, Holle Joseph amesema Dunga anapaswa kurejesha fedha hizo kabla ya Novemba 18 ili ziweze kurejeshwa kwa wakulima hao wawili wa Wilaya ya Hanang'.

Makungu amesema mkurugenzi wa kampuni hiyo Dunga alipewa fedha hizo na wakulima hao wawili ili awanunulie trekta ila fedha hizo zikaingizwa kwenye akaunti yake binafsi badala ya akaunti ya kampuni.

Amesema walipata malalamiko kwa wakulima wawili wa wilayani Hanang' walitoa shilingi milioni 17 na shilingi milioni 16.2 mwaka 2016 kuweka kwenye akaunti yake binafsi ya Dunga ili wanunuliwe matrekta mawili ila hadi sasa hawajapatiwa.

"Katika uchunguzi wetu Takukuru mkoani Manyara imebaini kuwa Dunga alielekeza fedha hizo kwenye akaunti yake binafsi badala ya kampuni jambo linaloashiria nia ovu na kwa sheria zilizopo anaweza kushtakiwa kwa makosa ya jinai yakiwemo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu au kutakatisha fedha hizo," amesema Makungu.

Amesema Oktoba 25 mwaka huu Rais John Magufuli akiwa kwenye uwanja wa Kwaraa mjini Babati moja ya ahadi zake ilikuwa kuhakikisha rushwa na dhuluma zinakomeshwa na ikatoa mwamko kwa wana Manyara waliodhulumiwa miaka ya nyuma kudai haki zao.

"Rais Magufuli katika awamu yake ya pili ya uongozi wa nchi hii aliahidi atahakikisha rushwa na dhuluma zinatokomezwa na sisi tunatekeleza hilo kwa kufanyia kazi taarifa hii hata kama imetokea muda mrefu kwani jinai haifi hadi mtenda jinai atangulie mbele ya haki," amesema Makungu.

Amemtaka Dunga popote alipo awasilishe fedha hizo kwa mkuu wa Takukuru kabla ya Novemba 18 ili ziweze kurejeshwa kwa wakulima hao na kushindwa kutekeleza agizo hilo bila shuruti kutalazimisha kuchukua hatua zaidi kwa misingi ya sheria zinazotawala eneo hilo.

"Ni rai yetu iwapo kuna wakulima wengine ambao fedha zao zilichukuliwa na Dunga kwa udanganyifu wakuletewa matrekta na hawakuletewa wawasilishe malalamiko yao kupitia namba yetu ya dharura 113 au simu ya mkononi 0738150124 ili yashughulikiwe kwa pamoja," amesema Makungu.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari.