Rais Donald Trump amemfuta kazi Waziri wa Ulinzi Mark Esper, na kutangaza kwenye Twitter kwamba afisa huyo wa ngazi ya juu wa Marekani “amefutwa”.

Christopher Miller, mkuu wa sasa wa Kituo Cha Kukabiliana na ugaidi amechukua nafasi hiyo mara moja.

Hii ni baada ya wawili hao kutofautiana hadharani katika wiki za hivi karibuni.

Bw. Trump mpaka sasa hajakubali kushindwa katika uchaguzi wa Marekani na rais mteule Joe Biden, na ameapa kupinga matokeo hayo mahakamani.

Wiki chache zilizosalia kabla ya Biden kuchukua ofisi Januari 20, Trump bado ana uwezo wa kufanya maamuzi.

Rais Trump alitangaza kwamba Christopher Miller atakuwa waziri mpya wa ulinzi
Rais Trump alitangaza kwamba Christopher Miller atakuwa waziri mpya wa ulinzi

Bw Miller alionekana akiingia makao makuu ya kitengo cha ulinzi Pentagon siku ya Jumatatu muda mfupi kabla ya Bw. Trump kutangaza kufutwa kwake.

Afisa huyo wa zamani wa vikosi maalum alihudumu katika baraza la usalama la kitaifa la Rais Trump kabla ya kuwa mkuu wa Kituo cha kukabilina na ugaidi mwezi Agosti.

Katika barua ya kuacha kazi, Bw Esper aliwashukuru maafisa wa vikosi vya jeshi na kusema kwamba anajivunia yale aliyoweza kufikia katika kipinĸi cha miezi 18 alichohudumu Pentagon.

“Nilihudumia nchi yangu kwa mujibu wa katiba, kwa hivyo nakubali uamuzi wako wa kumleta mtu mwingine kuchukua nafasi hii ,” aliandika.

Mwanasiasa wa ngazi ya juu wa Chama cha Democratic Nancy Pelosi amekosoa uamuzi huo.

“Kufutwa ghafla kwa waziri Esper ni ishara wazi kwamba Rais Trump ana lengo la kutumia siku zake za mwisho ofisini kuvuruga demokrasia ya Marekani na sehemu nyingine duniani,” alisema spika huyo wa Bunge la Wawakilishi.

Kwa nini Trump alikosana na waziri wake wa ulinzi?

Bwana Esper alitofautiana na rais kufuatia muenendo wa White House kwa majeshi wakati wa maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi mapema mwaka huu.

Wakati Marekani ilipokumbwa na maandamano makubwa kufuatia kifo cha mtu mweusi George Floyd mikononi mwa polisi mjini Minneapolis, Minnesota, mwezi Mei, Bw. Trump alitishia kutumia wanajeshi kuvunja maandamano hayo.

Mwezi Juni, Bw. Esper, afisa wa zamani wa jeshi alisema hakuna haja ya kutumia jeshi, tamko ambalo limasadikiwa halikuridhisha White House.

Kufuatia tofauti hizo, kulikwa na fununu kwamba rais huenda akamfuta kazi Waziri wa Ulinzi, japo siku ya Jumatatu Trump hakutoa sababu ya kumfuta.

Bw. Esper pia ametofautiana na Trump kuhusu hatua ya rais kupuuza shirika la kujihami la nchi za magharibi, Nato.

Katika mahojiano na gazeti la Military Times wiki iliyopita , Bw. Esper alisema licha ya kuwa na uhusiano mgumu na White House, hakuamini kuondoka ni hatua nzuri.

“Rais amekuwa wazi kuhusu kile anachotaka. Na amekuwa wazi kuhusu maoni yake… sijaribu kumfurahisha mtu yeyote,” aliambia mtandao huo.

“kile ninacho jaribu kufanya ni, kutimiza anachotaka — kwasababu amechaguliwa na ndiye kamanda mkuu wa majeshi.”

Rais Trump amewafuta kazi maafisa kadhaa na washauri wakati wa utawala wake, mara nyingi kupitia ujumbe wa Twitter.

Mtangulizi wa Bw. Esper alikuwa James Mattis, ambaye alijiuzulu mwaka 2018 baada ya kutofautiana na rais kuhusu masuala tofauti ikiwemo vita vya Syria.

Wakati wa maandamano ya mwezi Juni, dhidi ya ubaguzi wa rangi, Bw Mattis alimkosoa Donald Trump akisema ni ” rais wa kwanza katika maisha yangu ambaye hataki kujaribu kuunganisha watu wa Marekani – wala hajifanyi kuwa anajaribu. Badala yake anajaribu kutugawanya.”

https://www.instagram.com/tv/CHZgiC6B002/

https://www.instagram.com/tv/CHZgiC6B002/

The post Donald Trump amfuta kazi Waziri wa Ulinzi Mark Esper, sababu zaelezwa appeared first on Bongo5.com.