Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema shughuli ya kuapishwa kwa Rais Mteule wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi na Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Magufuli zitafanyika wiki ijayo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za chama hicho jijini Dar es Salaam Polepole amesema Dkt. Mwinyi ambaye alishinda katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, 2020 ataapishwa Novemba 2, 2020 katika Uwanja vya Amani Zanzibar kuwa Rais wa awamu ya nane wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya rais Dkt. Ali Mohamed Shein kumaliza muda wake.

Siku mbili zimepita tangu Tume ya ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kumtangaza Dkt. Mwinyi kuwa mshindi wa kiti cha urais kwa kujipatia kura 380,02 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote halali.

Kwa upande wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, Polepole amebainisha kuwa shughuli ya kuapishwa kwake kuongoza dola kwa muhula itafanyika Novemba 5, 2020 katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Dkt. Magufuli alitangazwa kuwa mshindi baada ya kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali.

Katibu mkuu huyo amewashukuru Watanzania wote kwa kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukipatia ushindi wa kishindo, hivyo kuwataka kujitokeza kwa wingi katika matukio hayo muhimu la kuapishwa kwa viongozi wateule
.