Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Halima Mdee na wenzake 18 wamevuliwa uanachama wa chama hicho kwa sababu wamekiuka katiba na kanuni za chama hicho kwa uamuzi wao wa kwenda kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum bila chama hicho kuwapitisha.
Mbowe ametoa tamko hilo jana Ijumaa Novemba 27, 2020 saa 5 usiku wakati akisoma maazimio ya kikao cha kamati kuu kilichoketi kuanzia saa 3 asubuhi kuwajadili wabunge hao.
Waliovuliwa uanachama ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnesta Lambart, Nusrati Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Nagenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Fiao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.
Kabla ya kutangaza uamuzi huo, Mbowe alitaja hatua nyingine tatu ambazo kamati kuu imezichukua ikiwa ni pamoja na kuwavua nyadhifa miongoni mwao waliokuwa viongozi wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) na lile la wanawake (Bawacha) na kuagiza mchakato wa kujaza nafasi zao uanze mara moja.
”Chama chetu hakijateua Wabunge wa Viti Maalum tunaona tu Watu wetu wanaapishwa na hatuna taarifa, hatujapeleka majina, fomu za Tume zipo ofisini Mama zetu hawa Dada zetu hawajajaza fomu, ila tunaona tu wanaapishwa” Mbowe
“Kamati Kuu imewavua Uongozi wale wote ambao walikuwa Viongozi kwenye Mabaraza kati ya hao Dada zetu 19 sitaki kupoteza muda kuwataja majina, kwahiyo kuanzia sasa hawapaswi kushughulika na lolote kama Viongozi na tumeelekeza nafasi zao zizibwe haraka” Mbowe