Dodoma. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally  amesema chama hicho kimeongeza siku moja ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuomba kuteuliwa kuwania uspika na unaibu.


Awali, chama hicho tawala kilieleza kuwa shughuli ya kuchukua fomu ingefanyika kwa siku mbili kuanzia jana hadi leo Jumanne Novemba 3, 2020 saa 10 jioni lakini Dk Bashiru amesema mwisho itakuwa kesho saa 10 jioni.


Amesema kwa upande wa Baraza la wawakilishi Zanzibar kazi hiyo imefungwa leo Novemba 3,2020 na wanachama watano wamechukua fomi.


Amesema baada ya shughuli hiyo kufungwa,  Novemba 6, 2020 kamati kuu ya halmashauri ya Taifa  itakutana kwa ajili ya kupokea taarifa ya awali ya utekelezaji wa mpango wa uchaguzi mkuu 2020, pamoja na  kupitia maombi ya wanachama wa CCM wanaoomba kushika nafasi za uspika katika baraza la uwakilishi Zanzibar na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Kuhusu wanaoomba nafasi za uongozi ngazi ya wenyeviti wa halmashauri za miji na wilaya, Meya wa manispaa na majiji amesema wataendelea kuchukua fomu hadi Novemba 5, 2020  saa 10 jioni.


Amesema baada ya hapo kamati kuu itatoa ratiba ya vikao vya uteuzi kuanzia ngazi za kamati za siasa wilaya hadi mkoa na itazingatia muda wa kutosha wa kupitia  maombi hayo ili baadaye kamati kuu iweze kupitia na kuthibitisha maamuzi yaliyofanywa na kamati hizo.


“Hii itakiwezesha chama kupima sifa za waombaji ili kupendekeza  viongozi ambao wataweza kusimamia halmashauri na manispaa.”


“Uzoefu unaonyesha kuwa Serikali ilikuwa inatenga fedha za maendeleo nyingi na kuna wakati ambao  usimamizi ulikuwa una lega lengo sasa kimeamua kufanya hivyo ili kuwa na safu ya uongozi ambao utasaidia usimamizi wa fedha za miradi , uwajibikaji  na kukifanya chama kuwa karibu na wananchi,” amesema Dk Bashiru.