Leo ni siku ya pili ya zoezi la uteuzi wa wagombea wa kiti cha urais nchini Uganda, ambapo mpinzani mkuu Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine anatarajiwa kuteuliwa.

Bobi Wine (kushoto) anatarajiwa kuteuliwa kuwa mgombea urais hii leo

Kulingana na mwandishi wa BBC Issaac Mumena, Bobi Wine anatarajiwa kuteuliwa majira ya asubuhi.

Wakati huohuo Ubalozi wa Marekani Kampala umetoa tahadhari ya usalama kwa raia wake mjini Kampala.

Ubalozi huo umeshauri raia wake kujizuia kufika maeneo ya mji wa Kampala na karibu na eneo la Kyambogo kwasababu ya uwezekano wa kutokea kwa ghasia Jumanne kunakohusishwa na shughuli ya uteuzi wa urais.

Kabla ya kutoka nyumbani kwake, Bobi Wine alisema kuwa atazungumza na vyombo vya habari na amekubali kwenda na watu 10 kama inavyotakiwa na Tume ya Uchaguzi ya Uganda.

Hata hivyo, inasemekana kwamba jeshi la polisi limezunguka ofisi za chama cha Bobi Wine cha National Unity Platform, NUP.

Pia hali ya usalama imeimarishwa katika mji wa Kampala na vitongoji vyake.

Hapo jana rais Yoweri Museveni alikuwa miongoni mwa walioteuliwa na kupata fursa nyengine ya kutetea kiti chake kwa muhula mwingine

The post Bobi Wine kuteuliwa kugombea urais leo appeared first on Bongo5.com.