Mwenyekiti wa Baraza la vijana (BAVICHA) Jimbo la Shinyanga mjini Samson Ng'wagi, katikati, akizungumza na waandishi wa habari, kushoto ni Mwenyekiti wa BAWACHA Jimbo la Shinyanga mjini Zena Gulam, na kulia ni Katibu mwenezi wa BAVICHA, Ibrahimu Isack.

Na Marco Maduhu Shinyanga

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema (BAVICHA) jimbo la Shinyanga mjini, limemtaka aliyekuwa mwenyeki wa Baraza la wanawake Chadema Taifa (BAWACHA), Halima Mdee, pamoja na wenzake 18 wakiombe radhi chama hicho.

Mwenyekiti wa baraza hilo Samson Ngwa'gi, amebainisha hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Chadema Kanda ya Serengeti.

Amesema kitendo alichokifanya Halima Mdee pamoja na wenzake 18 kukisaliti chama, na kwenda bungeni Jijini Dodoma kuapishwa kuwa wabunge viti maalum ni kosa kubwa, na wamestahili kuadhibiwa na kamati kuu.

"Baraza la vijana jimbo la Shinyanga mjini, tunaunga mkono maamuzi yaliyotolewa na kamati kuu ya kuwavua nyadhifa zao na uanachama Halima Mdee pamoja na wenzake 18," amesema Ng'wagi.

"Pia tunawaomba wafuate maagizo ambayo yametolewa na Kamati kuu dhidi yao, ya kuomba radhi ama kukata rufaa, tunataka chama chetu tuendelee kuwa imara na tusigawanyike kwa maslahi binafsi," ameongeza.

Pia amesema ndani ya chama hicho hakuna mfumo dume ambao umedaiwa kuwepo na Halima Mdee, na kueleza kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu uliopita, chama hicho ndicho kilipitisha wagombea wengi wa nafasi ya ubunge ambao ni wanawake.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la wanawake jimbo la Shinyanga mjini (BAWACHA) Zena Gulam, ameeleza kusikitishwa na kitendo ambacho amekifanya Halima Mdee, akidai kuwa ni kiongozi ambaye alikuwa akimfuata nyayo zake, lakini kwa tukio hilo limemvunja moyo.

Novemba 24 Halima Mdee pamoja na wenzake 18, walikwenda Bungeni jijini Dodoma na kuapishwa kuwa wabunge viti maalum kupitia Chadema, lakini Novemba 27 wakafukuzwa uanachama na kamati kuu ya Chama hicho, wakidaiwa kukisaliti chama, kwa madai hawakuteuliwa kuwa wabunge wa viti hivyo ndani ya chama.
Mwenyekiti wa Baraza la vijana (BAVICHA) Jimbo la Shinyanga mjini Samson Ng'wagi, katikati, akizungumza na waandishi wa habari, kushoto ni Mwenyekiti wa (BAWACHA) Jimbo la Shinyanga mjini Zena Gulam, na kulia ni Katibu mwenezi wa BAVICHA, Ibrahimu Isack.Mwenyekiti wa (BAWACHA) Jimbo la Shinyanga mjini Zena Gulam, akizungumza kwenye kikao hicho.