KIUNGO msumbufu wa Simba, Luis Miquissone, juzi akiwa kwenye majukumu yake ya timu ya Taifa ya Msumbuji alikuwa kwenye wakati mgumu baada ya jitihada zake za kutimiza majukumu yake kugonga mwamba.


Luis ambaye ni mchezaji wa Simba akiwa ni kinara wa kutoa pasi za mwisho akiwa nazo sita na amefunga bao moja ndani ya ligi alikuwa kwenye wakati mgumu wakati akishuhudia timu yake ikipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Cameroon, Uwanja wa Estadio do Zimpeto.


Takwimu zinaonyesha kwamba dakika ya 20 Luis alisababisha penalti kwa timu yake ya Taifa ya Msumbiji baada ya kuchezewa faulo ndani ya 18, penalti ilipigwa na Reginaldo Faife alikosa kwa kugongesha mpira kwenye mwamba na kufanya timu yake ishindwe kupata bao la mapema.


Dakika ya 39 alichezewa faulo ambayo haikuleta matunda na dakika ya 57 alitengeneza nafasi ya wazi ya bao ambayo mchezaji mwenzake Stanley Ratifo alikosa nafasi ya wazi ya kufunga ndani ya 18.


Dakika ya 75 alipiga shuti kali nje ya 18 kipa wa Cameroon alitema ikakutana na mchezaji yuleyule wa Msumbiji Ratifo ambaye alikosa mara ya pili na kuifanya timu yake kupoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Cameroon kwenye mchezo wa kuwania kufuzu Afcon.


 

Matokeo hayo yanaifanya Msumbuji iwe nafasi ya pili na pointi 4 huku Cameroon ambao tayari washafuzu michuano hiyo kwa kuwa ni wenyeji wapo nafasi ya kwanza na pointi zao ni 10 katika kundi F.