Tanzania na Malawi zimekubaliana kushirikiana kuboresha sekta za usafirishaji, uvuvi, madini, nishati, utalii na kilimo.
Makubaliano hayo yalitangazwa jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla maalum iliyohusisha marais wa nchi hizo mbili, mwenyeji Dk. John Magufuli na Rais Lazarus Chakwera aliyezuru nchini kwa ziara ya siku tatu.

Rais Magufuli alimshukuru Rais Chakwera kwa kuitembelea Tanzania na kuwa nchi ya tatu kutembelewa barani Afrika kwa kiongozi mpya wa Malawi baada ya Burundi na Uganda tangu aingie madarakani.

Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema nchi hizo mbili zina historia ya undugu kutokana na mwingiliano wa watu wake katika shughuli mbalimbali ikiwamo biashara.