I MEISHA hiyo! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya kufahamika kwamba, picha za kimahaba zinazosambaa za staa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu na kiungo nyota kutoka Angola, Carlos Guimaraes do Carmo Carlinhos, anayeichezea klabu ya Yanga ni za tangazo na kwamba hakuna chochote cha kimapenzi kati ya wawili hao
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, picha hizo hasa zile za kitandani na kwenye makochi, ni za matangazo ya fenicha za ndani zinazouzwa na kusambazwa na kampuni moja maarufu nchini. Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Wema anasema kuwa, picha hizo ni shughuli maalum (tangazo) na si kweli kwamba kuna chochote kinachoendelea kati yao.
“Ni picha maalum za project f’lani hivi na hakuna kingine kati yetu pamoja na kwamba mimi ni shabiki yake (Carlinhos) na timu yangu ya Yanga,” anasema Wema kwa kifupi.
Picha hizo za Carlinhos na Wema zimekuwa zikiibua gumzo miongoni mwa mashabiki wa Yanga (Wananchi), wengi wakijiuliza maswali juu ya namna walivyokutana. Ikumbukwe Wema mara baada ya usajili wa Carlinhos ndani ya Yanga, alisema kuwa angependa kuona Yanga inashinda mataji ya ligi mara saba ndipo mambo mengine yazungumzwe.
“Tunachotaka sisi tupate ubingwa, tena mara saba, halafu ndiyo tuanze kuongea lugha moja…na zitabaki saba hivyohivyo maana ubingwa ni wetu round hii, karibu sana Carlinhos,” alisema Wema.