Samirah Yusuph
Mgombea nafasi ya ubunge katika jimbo la Bariadi mkoani Simiyu kwa tiketi ya CCM Mhandisi Andrea Kundo amesikitishwa na hali ya watoto wa kike kushindwa kufikia ndoto zao kwa changamoto ya kuwa mbali na shule.

Mhandisi Kundo ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya Ihusi wilayani Bariadi alipokuwa katika mkutano wa kuomba ridhaa ya kuingia bungeni katika kata hiyo.

Alisema  licha ya kuwa amesoma katika mazingira hayo lakini tangu kipindi hicho hakuna maendeleo yoyote yanayo onyesha utatuzi wa changamoto hiyo hivyo ameahidi kufanikisha ujenzi wa shule ya sekondari katika kata ambapo mwanzo hapakuwa na shule ya sekondari.

"Ninatambua watoto wetu wanatembea umbali mrefu ili kwenda shule napengine wanakwenda kusoma katika shule za nje na kata hii hivyo inatakiwa hapa shule ipatikane na hilo litakuwa ni kipaumbele changu ndani ya miaka mitano ya mwanzo," alisema Mhandisi Kundo .

Hali hiyo ambayo imelezewa na wananchi kuwa nikikwazo kikubwa kinachopelekea watoto wengi kuwa watoro katika masomo yao na pengine kutokumaliza elimu yao ya sekondari hivyo wengi kubaki mtaa bila kuwa na kazi rasimi .

"Hali ni mbaya watoto wetu wanapitia wakati mgumu kwa sababu shule ipo mbali sana vilevile katika msimu wa mvua inakuwa ni shida kwa sababu kuna mito mingi ambayo inajaa maji na kuwafanya washindwe kwenda shule ," alieleza Gilasi Masunga .

Kata hiyo imezungukwa na mito mikubwa mitatu ambayo msimu wa mvuwa inajaa maji hivyo wanafunzi hawawezi kupita kwenda shule kata ya jirani ambayo ni Nkololo huku wanafunzi wengine wakisoma katika kata ya Nkindwabiye.

"Wanangu wanasoma Nkindwabiye lakini huyo wa kike ninakuwa na wasiwasi naye sana kwa sababu huko amepanga chumba hali ambayo sijui usalama wake kwa sababu bado ni mdongo na huko lazima aende ili akasome,"alisema Kwandu Masahi.

Hollo Ngisa yeye alisema kuwa " inakuwa ni ngumu mtoto kuruhusu mtoto kwenda shule kwa sababu ya shule zipo mbali na wanachelewa sana kurudi nyumbani hivyo ni bora akae afanye kazi za nyumbani ," .

Kata ya Ihusi haijawahi kuwa na shule ya sekondari hivyo wanafunzi wengi humaliza elimu ya msingi na baadhi yao ndiyo hupata nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na wingi wa changamoto zinazowakabili hivyo wamemuomba mgombea ubunge( ccm) katika jimbo hilo kuhakikisha pindi atakapoingia madarakani ahakikishe anafuta kilio chao .

Mwisho.