Jeshi la Polisi linawashikilia viongozi watano wa Chadema katika kata ya Gwanumpu  wilayani Kakonko kwa tuhuma za kukutwa na vitambulisho 14 vya wapigakura, kinyume cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.

Akizungumza  Oktoba 21, kamanda wa polisi wa mkoa, James Manyama amesema tukio hilo lilitokea j Oktoba 20, saa 10:00 jioni katika duka la kuuuza vifaa vya shule na ofisi katika kijiji cha Kakonko.

Amesema polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ambao walikuwa katika operesheni ya kuzuia na kukamata wahalifu, walikamata watuhumiwa hao watano wakiwa na kadi hizo.

Amesema watu hao wamevunja Sheria ya Uchaguzi, sura ya 343 na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Akizungumzia suala hilo, katibu wa Chadema mkoa, Shaban Madede amesema viongozi hao walienda kutoa nakala za vitambulisho vya kupigia kura vya mawakala wao na kwamba wangevirudisha baadaye.