ROBERT Sylvester Kelly ‘R-Kelly’ alizaliwa Januari 8, 1967 Chicago, nchini Marekani. Katika familia yao R-Kelly alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto wanne.


Mama yake ‘Joanne Kelly’ alikuwa mwimbaji, kiongozi wa kwaya aliyewalea watoto wake katika maadili ya kanisa la Baptist huku Baba yake R-Kelly hakufahamika wala kuonekana kipindi chote cha malezi.


R-Kelly sio jina geni masikioni kwa wapenzi wa burudani ya muziki ulimwenguni kutokana kazi zake za uimbaji, utunzi na utayarishaji wa muziki zilizompa umaarufu na kupachikwa majina kama vile “Mfalme wa R&B”, “Mfalme wa Pop-Soul” na “Pied Piper of R&B” pia anasifi ka kwa kufufua tena muziki wa R&B na hip hop nchini Marekani.

Kwa sasa msanii huyo amepoteza mwelekeo kutokana na mambo mbalimbali yaliyomsibu. Makala hii inakupakulia undani wa chanzo cha kupanda na kushuka kwa R-kelly.


 


AANZA KUIMBA NA MIAKA NANE


Kutokana na malezi ya mama yake ambaye alikuwa ni kiongozi wa kwaya, R-kelly alianza safari yake ya muziki kwa kuimba kwaya kwenye kanisani hilo akiwa na umri wa miaka nane na huko ndiko kipaji chake kilipolelewa kisha baadae kuanza kuimba R&B na HIPHOP.


 


AFANYIWA UDHALILISHAJI WA KINGONO UTOTONI


R-Kelly alikua katika nyumba iliyojaa wanawake. Katika maelezo yake alisema mambo yalikuwa yakifanyika tofauti wakati mama yake na babu yake hawapo nyumbani.


 


Alipokuwa na umri wa miaka 10, R-Kelly alinyanyaswa kingono na mwanamume mkubwa ambaye alikuwa rafi ki wa familia na alipofi kisha umri wa miaka 14 alinyanyaswa kingono na mwanafamilia wa kike aliyemzidi umri.


 


Katika kitabu cha wasifu wake alichokitoa mwaka 2012 alisema kwamba «alikuwa na hofu na aibu sana ndiyo maana hakuweza kumwambia mtu yeyote.


 


ALIVYOINGIA KWENYE MUZIKI


Ndoto za R-Kelly zilikuwa ni kuja kuwa mchezaji wa mpira wa kikapu (Basketball). Mchezo ambao ni maarufu nchini Marekani.


 


Hata hivyo, haikuwa rahisi kwake kupenya kwenye fani hiyo na mwaka 1983 alikutana na Mwalimu wa muziki, Lena McLin, ambaye alimhimiza Kelly kuigiza kwenye tamasha la Stevie Wonder classic «Ribbon in the Sky» katika onyesho la talanta.


 


Kelly alipanda jukwaani na kuimba wimbo uliompa fursa ya kushinda tuzo ya kwanza hali iliyomfanya akabadilisha mawazo.


 


MUZIKI WAMPANDISHA LEVO ZINGINE


Baada ya kuingia kwenye muziki, nyota ya R-Kelly iling’ara kupita maelezo na mwaka 1989 alianza kushinda kwenye shindano la ‘Big break’ lililokuwa linafuatiliwa na watu wengi Marekani ambapo alivuna mkwanja mrefu.


 


Alipofi ka miaka ya 1990 R-Kelly alivunja rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa kiume aliyefanikiwa zaidi ulimwenguni baada ya kuuza ‘singo’ milioni 75 na kuuza album milioni 32, alitajwa na Billboard kama Msanii wa Juu wa R & B na Hip Hop kati ya 1985-2010 na msanii aliyefanikiwa zaidi wa R&B katika historia.


 


Mwaka 2010 R-kelly alipata nafasi ya kuimba wimbo wa “Sign of a Victory” katika sherehe za ufunguzi wa kombe la dunia mwaka 2010.


 


AJIOKOTEA TUZO ZA GRAMMY


Kupitia album kali za R-Kelly amefanikiwa kutwaa tuzo mbalimbli za Grammy na nyinginezo nyingi ulimwenguni. Mwaka 1995, Kelly alipata uteuzi wake wa kwanza wa Grammy kwa kuandika, kutengeneza na kutunga wimbo wa mwisho wa Michael Jackson «You are not alone», Mwaka Novemba 26, 1996, Kelly aliachia “I believe i can fl y”, wimbo wa kuhamasisha uliotolewa mwanzoni kwenye wimbo wa filamu ya Space Jam ambao ulishika namba moja kwenye chati za Uingereza kwa wiki tatu na kushinda Tuzo tatu za Grammy mwaka 1998.


 


MIKASA YAANZA KUMPOTEZA


Licha ya R-Kelly kufi kia levo za juu za mafanikio kwa sasa hali yake ya kiuchumi imeporomoka na kesi kibao za udhalilishaji wa kijinsia zinamtafuna. Ifuatayo ni mikasa iliyochangia.


 


AFUNGA NDOA ISIYOHALALI KISHERIA


Mwaka 1994, R-kelly aliyekuwa na miaka 27 alimuoa kwa siri mwanadada ‘Aaliyah’ mwenye umri wa miaka 15. Taarifa iliyoripotiwa na Chicago Sun-Times, mwaka 2008 katika mahojiano Aaliyah alikiri alikuwa amesema kwa uwongo. Ndoa ilifutwa Februari mwaka 1995 kwa amri ya familia ya Aaliyah na jaji wa Michigan.


 


MADAI YA PONOGRAFIA KWA WATOTO


Mwaka 1998, Kelly alidaiwa kumlipa Tiffany Hawkins dola za Marekani 250,000 baada ya kumshawishi kufanya ngono na kikundi cha vijana wengine wakati alikuwa na umri wa miaka 15.


 


Mwaka Februari 3, 2002, video ilionekana ikimwonyesha Kelly akifanya mapenzi na msichana mdogo, Kelly alikana kuwa hakuwa yeye katika video hiyo. Juni mwaka 2002, R-Kelly alishtakiwa huko Chicago kwa makosa 21 ya ponografi a ya watoto na mwezi huo huo, alikamatwa na idara ya Polisi ya Miami kisha baadaye aliachiliwa dhamana.


 


ATUPWA GEREZANI BILA DHAMANA


Mnamo Juni, 2019 alikamatwa na kuwekwa gerezani bila dhamana kwa makosa mawili yanayohusiana na unyanyasaji wa kingono na mashtaka kadhaa yanayomkabili yaliyowasilishwa kipindi cha nyuma katika kaunti ya Cook.


 


ASHAMBULIWA GEREZANI


Agosti mwaka huu, Wakili wake alidai kuwa R-Kelly ameshambuliwa na mfungwa mwingine gerezani. Inasemekana alishambuliwa katika Kituo cha Marekebisho ya Metropolitan huko Chicago, ambapo anasubiri kesi baada ya kukataa kushtakiwa kwa mashtaka kadhaa ya uhalifu wa kijinsia.