Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amesema, uamuzi uliofanywa na Kamati ya Maadili ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wa kumsimamisha kufanya kampeni siku saba haukuzingatia utaratibu wa kisheria na kanuni.
Amesema, amehukumiwa bila kupewa tuhuma kwa maandishi, kuwasilisha utetezi wake na kusikilizwa kama Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ya Urais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020 zilizotolewa na NEC zinavyoelekeza.

Uamuzi wa kamati ya maadili umetolewa jana Ijumaa tarehe 2 Oktoba 2020 na Emmanuel Kawishe, Katibu wa kamati hiyo ukionyeshwa Lissu amesimamishwa kufanya kampeni kwa siku saba kuanzia kesho Jumamosi hadi 9 Oktoba 2020.

Kawishe amesema, Lissu amekutana na kadhia hiyo baada ya malalamiko yaliyowasilishwa na chama cha NRA na Chama Cha Mapinduzi (CCM) vikimtuhumu kutoa mameno ya uchochezi yasiyothibitika.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Tegeta jijini Dar es Salaam jan Ijumaa , Lissu alisema muda huo  (ilikuwa saa 11 jioni) hajapewa malalamiko yoyote ya maandishi ya hivyo vyama NRA na CCM kinyume cha kanuni za maadili ya uchaguzi.

Alisema, kutokana na uamuzi huo, Kamati Kuu ya Chadema inakutana leo katika kikao cha dharula kujadili suala hili na kutoa uamuzi.
 
"Kamati kuu ya chama chetu inakutana kesho(leo) ili kulijadili suala hili na kulitolea ufafanuzi,msimamo wangu binafsi ni kwamba kampeni zinaendele siku ya jumapili kama mabavyo imepangawa kwenye ratiba iliyoratibiwa na tume ya taifa ya uchaguzi kwa hiyo msimamo ndio huu" alisema Lissu