Sifa ya Tanzania Duniani ni Umoja na Mshikamano – Rais Magufuli
Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watanzania kuendelea kudumisha tunu ya umoja na mshikamano iliyoasisiwa na waasisi wa Taifa hili na kamwe wasikubali kuibomoa iwe kwa dini au kabila.
Akizungumza jana (Jumatatu, Oktoba 26, 2020) wilayani Chamwino mkoani Dodoma, wakati akizindua msikiti wa Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally Rais Magufuli alisema kuwa msikiti huo utumike kuwaweka pamoja kama ndugu, pia ukawe fundisho kwa wana Chamwino na watanzania katika kuwa wamoja na kutambua kuwa wana wajibu wa kumtanguliza Mungu katika maisha yote.
“Msikiti huu ukatoe mafunzo yatakayojenga umoja wa watanzania, ukaguse na mioyo yao ya kutekeleza maandiko matakatifu yaliyopo kwenye Quran na yakajenge umoja ndani ya watanzania wote,” alisisitiza.
Aliongeza “ishara hii mliyoionyesha leo ni ya kipekee duniani kote, upendo huu na umoja huu ni wa maajabu sana, tuendelee kushikamana”
Aidha, Rais Magufuli aliwakumbusha watanzania kwenda kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu kulingana na utashi wa mioyo yao kwa kuchangua viongozi watakaoweka mbele maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Meja Jenerali Charls Mbuge alisema kuwa msikiti huo wenye ofisi ya Mufti umejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 319.28 umekamilika kwa asilimia 100.
“Endapo msikiti huu ungejengwa na mkandarasi basi ungetumia shilingi milioni 439.43, na umekamilika kwa asilimia 100 na tumeujenga kwa mwezi mmoja na siku 28 tu.”
Aidha, Meja Jenerali Mbuge, amemshukuru Rais Magufuli kwa kuifanya JKT kuwa karibu na wananchi na kuahidi kuendelea kutekeleza maagizo pamoja na majukumu yao kwa ufanisi.
Naye Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi alimshukuru Rais Magufuli kwa kuwajengea msikiti wenye hadhi na sambamba na uamuzi wake wa kurudisha mali za waislamu zilizopotea.
“Umekuwa kiongozi mwenye kipaji cha kupenda viongozi wa dini na mwenye kumtanguliza Mungu katika Kila jambo. Vitabu vya Mungu vinasema anayefanyia wema mlipeni na kama hamna cha kumlipa muombeeni.”
Aidha, Mufti Zuberi alitumia fursa hiyo kuwataka watanzania kujitokeza kupiga kura kwa amani na utulivu, huku wakiendelea kuliombea taifa hata baada ya Uchanguzi Mkuu kumalizika.
Itakumbukwa kuwa Agosti 23, 2020, Rais Magufuli aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa msikiti wa Chamwino katika misa takatifu ya uzinduzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Immaculata Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, ambapo shilingi millioni 25.6 zilipatikana.