Jeshi la Marekani limesema limefanya shambulizi la ndege inayoruka bila ya rubani dhidi ya viongozi wa Al-Qaeda huko kaskazini magharibi mwa Syria, karibu na eneo la mpaka na kuwauwa wapiganaji 14 wa jihad. 

Shirika la Syria linalofanya uangalizi wa haki za binaadamu limesema wapiganaji hao waliouliwa wanajumuisha raia wanne wa kigeni na makamanda sita. 


Taarifa ya msemaji wa kituo cha kuongoza mashambulizi ya kijeshi kwa upande wa Marekani Meja Beth Riordan pasipo kutaja athari za shambulizi hilo ilisema lililenga kundi la wafuasi wa al-Qaeda, katika mkutano wao wa viongozi waandamizi karibu na mji wa Idlib. 


Vita vya Syria ambavyo vilianza baada ya ukandamizaji wa serikali dhidi ya waandamanaji 2011, vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 380,000 na wengine mamilioni kuachwa bila ya makazi.