Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji, Mhe. Angellah Kairuki  wamefanya kikao cha pamoja na wazalishaji wa saruji nchini kwa lengo la kujadili fursa mbalimbali, changamoto na namna bora ya kukuza sekta ya ujenzi nchini kupitia saruji, kikao kilichofanyika Ofisi za Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), jijini Dar es Salaam jana 17.10.2020

Katika kikao hicho, Mawaziri hao wamekutana na kampuni 9 za saruji zikiwemo Dangote Cement, Camel Cement, Nyati Cement, Mbeya Cement, Kilimanjaro Cement, Maweni Cement, Tanga Cement, Lake Cement, Twiga Cement pamoja na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI), wakijadili namna bora ya kuendeleza sekta hiyo.

Waziri Bashungwa aliwapongeza wazalishaji hao kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwasihi wasipandishe bei ya saruji kiholela hasa kuzingatia kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya 5 ni kuiona Tanzania inakua nchi ya viwanda.

Wazalishaji hao walizungumzia changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwemo ubovu wa barabara hasa kipindi cha mvua, unaofanya bei kuwa juu kidogo, upatikanaji wa nishati madhubuti kama gesi, suala la kodi na kuiomba serikali sikivu kushughulikia changamoto hizo.

Nae, Waziri Kairuki alisema kuwa wizara yake na Wizara ya Viwanda wanafanya kazi kwa ukaribu na kuwatoa hofu wazalishaji hao wa saruji kuwa serikali ipo pamoja nao na inashughulikia changamoto zao na kuwahakikishia wizara yake yenye dhamana ya uwekezaji itahakikisha inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji hao.

Nae Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Innocent Bashungwa aliwahakikishia wazalishaji hao kuwa serikali ina angalia namna bora ya kuhakikisha gesi inapatikana kwa urahisi hasa kwa viwanda vilivyopo Ukanda wa  Pwani pia amewahakikishia kuwa changamoto nyingine ndogo ndogo atazishughulikia ndani ya wiki moja ijayo.