Rais wa zamani wa Burundi, Pierre Buyoya amehukumiwa na mahakama kuu ya nchi hiyo kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kupanga mauaji ya raisi wa kwanza wa Kidemokrasia wa nchi hiyo, Melchoir Ndadaye, Oktoba 21, 1993.

Buyoya, ambaye anatoka mbari ya Kitutsi, aliingia madarakani mwaka 1987 kwa msaada wa jeshi. Aliachia madaraka mwaka 1993, wakati Ndadaye, ambaye ni Mhutu, alipochaguliwa kuwa rais. Lakini Ndadaye aliuawa miezi minne baadaye katika jaribio la mapinduzi lililoongozwa na wanajeshi wa Kitutsi wenye msimamo mkali.

Mauaji hayo yalifuatiwa na miaka kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya makundi ya kimbari, vita ambavyo vilisababisha watu wanaokadiriwa kufikia laki 3  kuuawa.

Mbali na Buyoya, maofisa 18 wa vyeo vya juu jeshini na raia waliokuwa karibu na kiongozi huyo, wamepewa adhabu kama hiyo.

Watu wengine watatu walihukumiwa kwenda jela kwa miaka 20 kwa kushiriki katika uhalifu huo, huku waziri mkuu wa zamani, Antoine Nduwayo, akiachiwa huru.