SALVATORY NTANDU
Raia wa China Wang Tao (37) na Yasiri Mussa (26) Mtanzania wafanyabiashara wa Madini wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kahama kwa tuhuma ya kumiliki kiwanda cha kuchenjulia dhahabu bila kibali.

Mbele ya Hakimu Makazi wa Mahakama ya Wilaya Davidi Msalilwa,Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Athumani Kisango alisema kuwa wawili hao wanatuhumiwa kumiliki kiwanda hicho bila kibali kutoka kwa Ofisi ya Madini.

Alisema kuwa Watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Septemba 29 Mwaka huu katika eneo la Manzese majira ya usiku ambapo walikamatwa kwa Tuhuma ya kumiliki kiwanda hicho kinyume cha sheria ya Madini ya mwaka 2019.

Katika shauri hilo la jinai namba 269 la Mwaka huu Watuhumiwa hao wanadaiwa kukiuka kifungu cha 6 (1) (3)(b)(4) cha sheria ya Madini namba 123 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019.

Watuhumiwa hao wamekana shitaka hilo na shauri hilo limeahirishwa hadi Oktoba 21 mwaka huu itakapotajwa tena Mahakamani hapo.

Wawili hao Waliachiliwa huru kwa  dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na Mahakama hiyo.

Mwisho.