Nusu ya wakaazi wote wa jimbo lililojitangazia uhuru la Nagorno-Karabakh wamelazimika kuyahama makaazi yao kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya majeshi ya Armenia na Azerbaijan. 
 
Hakuna upande wowote unaoonyesha kuwa tayari kujitolea ili kusimamisha vita hivyo vipya vipya vilivyoanza tarehe 27 Septemba. 
 
Akizungumza leo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha serikali ya Urusi, Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo amesema kinachoendelea kati ya mataifa hayo ambayo yalikuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti, ni msiba mkubwa, kwa sababu kila upande umewapoteza watu, na mali nyingi imeharibiwa. 
 
Vikosi vya Azerbaijan vimeushambulia mji mkuu wa Nagorno-Karabakh wa Stepanakert usiku mzima wa kuamkia leo, na ving'ora vilivyokuwa vikilia kuwaweka watukatika hali ya tahadhari. 
 
Jimbo hilo ambalo wakaazi wake wengi ni wa jamii ya Armenia, lilijitenga na Azerbaijan mnamo miaka ya 1990, baada ya vita vilivyogharimu maiasha ya watu 30,000.

Source-DW