Mkali muziki wa Taarab hapa nchini Mzee Yussuf amempongeza msanii Ben Pol kwa uamuzi wa kubadilisha dini na kuwa muislam kisha ameahidi kujitolea na kumsaidia kumfundisha Qur'an ambapo ndani ya wiki mbili atakuwa ameshaijua na kusoma.

Mzee Yussuf amesema anampongeza  Ben Pol kwa uamuzi wa kuridhia kuhamia kwenye uislam bila ya kuwa na vishawishi kama mapenzi au kulazimishwa. 

"Kuingia au kutoka kwenye dini ni fikra, falsafa, utashi na uhiari wake, kama uingiaji wake kwenye Uislam haihusiani na vishawishi, mapenzi au kulazimishwa hatopata tabu kabisa ila kama maamuzi yake yatahusiana na hivyo vitu itampa tabu kidogo kwenye nafsi yake" amesema Mzee Yussuf 

"Namshauri ajitahidi kupambana, ajielewe, afahamu na asione tabu, pia nipo tayari kuwa karibu naye kwa ajili ya mambo fulani kama fikra, mawazo na elimu, kama nikipata namba yake basi nawapa wiki 2 ataweza kusoma Qur'an tena nitamsaidia bure maana kuslim haitoshi anatakiwa aelewe dini yake na aifahamu" ameongeza