Mchungaji Daudi Mashimo ambaye ni mlezi wa msanii Amber Rutty amesema anaomba msaada wa watanzania ili kuwachangia Amber Rutty na mumewe Said Aboubakar ambao wapo gereza la Segerea.

Akizungumza na EATV & EA Radio Digital, Mchungaji Mashimo  amesema alijitolea kuwadhamini Amber Rutty na mumewe kwa mara kwanza ila kwa kuwa hukumu iliyotoka sasa hivi ni kubwa hawezi  kuimudu peke yake ndiyo maana anaomba msaada.

"Nilivyowatoa mara ya kwanza niliwashauri na walikubali kubadilika hivyo wakaamua kujitenga na mambo yao ndiyo maana nimeamua kusimama tena kujaribu kutafuta njia ya kuwalipia faini ili kutoka gerezani, wale ni watu ambao wanastahili msaada tusiangalie ya nyuma kwani yameshapita" ameeleza Mchungaji Daudi Mashimo 

Aidha Mchungaji huyo ameongeza kuwa "Nawaomba watanzania wenyewe moyo wa upendo na furaha kama ikiwapendeza tuwalipie faini ili watoke gerezani na sio lazima hiyo pesa mnipe mimi, mnaweza mkaenda hata Mahakamani mkatoa hiyo pesa ili atoke" 

Siku ya Septemba 25, ilitoka hukumu ya kifungo cha miaka mitano jela na faini ya milioni 3 kwa kila mmoja kasoro James Delicious ambaye alihukumiwa miaka mitano na faini ya milioni 5.