Shughuli za utafiti na uchimbaji wa makaa ya mawe katika mkoa wa Ruvuma zinafanyika katika Wilaya ya Mbinga maeneo ya Mbalawala na Mbuyula, Wilaya ya Songea katika maeneo ya Muhukuru, Njuga na Mtyangimbole na Wilaya ya Nyasa maeneo ya Malini kata ya Mtipwili na Mbambabay. 

Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Jumanne Mohamed Nkana amesema Mkoa wa Ruvuma una hazina ya makaa ya mawe zaidi ya tani milioni 227 ambayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa miaka 300.

Kulingana na Nkana,tafiti za awali za makaa ya mawe zimefanyika katika maeneo ya Mbalawala Mbinga ambako imebainika kuwa na tani milioni 99.5, Mbuyula Mbinga tani milioni 15.1 na  Muhukuru Songea tani milioni 27.

Kwa mujibu wa Nkana tafiti katika eneo la Njuga  wilaya ya Songea kuna tani milioni 23, wilaya ya Nyasa maeneo ya  Malini tani kata ya Mtipwili milioni 29, kijiji cha Liweta Kata ya Mbaha tani milioni 34.

Amesisitiza kuwa ubora wa makaa ya mawe yanayopatikana kwenye maeneo hayo yana wastani wa Calorific Value (CV)5,000 hadi 7,000.

Hata hivyo Afisa Madini Mkazi huyo wa Mkoa wa Ruvuma amesema uchimbaji mkubwa wa makaa ya mawe unafanyika katika maeneo ya Mbalawala,Mbuyula, Mbambabay, Muhukulu na Liweta.

Amewataja wateja wakubwa wa makaa ya mawe   yanayochimbwa katika maeneo hayo kwa sasa kuwa wapo ndani ya nchi na katika nchi jirani za Rwanda, Kenya na Uganda na kwamba wanatarajia kuanza kuuza makaa ya mawe katika nchi ya India.
Kwa upande wake  Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme ameziagiza kampuni zinazochimba makaa ya  mawe mkoani humo  kuuza makaa ya mawe kwenye viwanda vya ndani ili kupata nishati ya kutosha na ziada inayobaki isafirishwe kwenda nje ya nchi.
Mndeme pia ameziagiza  Kampuni hizo kutoa ajira kwa Watanzania ili waweze kunufaika na rasilimali za nchi huku akisisitiza kuchimba makaa ya mawe yenye viwango ili soko lipanuke, na kuzingatia usalama na afya za watumishi wote wanaofanya kazi katika migodini.
Maamuzi ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Magufuli Kuzuia kuagiza makaa ya mawe toka nje,badala yake watumiaji wote kutumia makaa ya mawe ndani ya nchi,hususani toka  Mkoani Ruvuma, kumesababisha soko la makaa hayo kupanda na kutoa ajira kwa watanzania.