Na Mwandishi wetu✍🏽


CHADEMA ni chama kinachojinasibu kwamba kinatetea uhuru wa kujieleza, kwamba ni chama ambacho kikiigia madarakani kitadumisha demokrasia, na kimekuwa mstari wa mbele kushutumu serikali kwamba inaminya hiyo demokrasia wanayoitaka na kuahidi kuitetea.


Lakini Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, akiongea na waandishi wa habari kuhusu adhabu ya mgombea wao kusimamishwa kampeni kwa siku saba, amesema kwa ujasiri kabisa kwamba kati ya vyama 15 vyenye wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu, vyama vingine vya upinzani vinamnyima haki mgombea wake wa urais, kwa sababu vyama hivyo havina msingi wala sababu ya kuwepo.


*_”Msijaze akilini mwenu kwamba kuna vyama vya siasa hapa, ni vitaasisi vinavyotafuta maslahi kupitia jukwaa la siasa, ndiyo wanaovuruga demokrasia katika taifa hili ni maadui wa demokrasia. Vinatupa shida kupanga ratiba yetu, tunaweza kuomba mgombea wetu  (Tundu) Lissu arudi Morogoro tunaambiwa pale kuna chama cha TADEA, mnataka kwenda Iringa mnaambiwa kuna chama kinaitwa SAU. Vyama hivi vinamyima haki mgombea wetu mwenye mamilioni ya wafuasi.”_*


Wakati Mbowe akisema haya, Ilani ya Chadema ya mwaka 2020, katika utangulizi wake imenukuu moja ya vipaumbele ni kusimamia utekelezaji wa madhumuni ya chama hicho kama yalivyoainishwa katika Ibara ya 4.1.4 ya Katiba ya Chadema  kwamba;


*_”Kuendeleza na kudumisha Demokrasia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, kujenga utamaduni wa demokrasia katika jamii kwa kutambua haki za wengi katika maamuzi; na pia kutambua haki za wachache kusikilizwa, kuheshimiwa na kulindwa, sambamba na kukubali ushindani huru, wa haki na wa wazi katika uchaguzi.”_*


Kauli ya Mbowe inazungumzia demokrasia gani kuhusu vyama vingi? Kwamba kwa Chadema demokrasia ya vyama vingi ni haki kwa chama chao na mgombea wao, vyama vingine vyote havina haki hiyo?


Inatisha kidogo wakati madhumuni ya Katiba ya Chadema yaliyofanywa kipaumbele kwenye ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu inasema kudumisha demokrasia, kutambua haki ya wengi na haki ya wachache kusikilizwa, kulindwa na kuheshimiwa, 

*_ameonyesha rangi zake halisi wasivyo na uvumilivu na walio kinyume chao._*


Mbowe na Chadema tafsiri yenu ya kuhesmimu na kulinda haki za wachache ni ipi? Mlitaka nini! Tume ya Uchaguzi isivipangie vyama hivi ratiba ya kampeni wakati vina wagombea walioomba nafasi ya kugombea kwa kufuata taratibu zote zinazotakiwa.


Najaribu kufikiria serikali ya Chadema ingekuwa na uvumilivu kiasi gani katika mfumo huu wa vyama vingi, sasa hivi mkiwa wapinzani tayari mnaona mna haki zaidi kuliko vyama vingine vyote, itakuwaje mkionja mamlaka?


Kwa maana nyepesi kabisa Mbowe anatuambia kuwa wanachama wa Chadema ndiyo Watanzania wenye haki zaidi kuliko wa NCCR – Mageuzi, CUF, TADEA na wasiokuwa na vyama.

Huu ni ukaburu kama ulivyo ukaburu mwingine, ni ubaguzi hatari kwa taifa letu, ambao hauna nafasi katika taifa hili.


*Magufuli mitano tena*