MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka mitano, Serikali imetumia sh. bilioni 5.26 kwa ajili ya ununuzi wa dawa kwenye Manispaa ya Lindi.

“Serikali imetoa shilingi bilioni 5.26 ambapo kati ya hizo, shilingi bilioni 4 zilikuwa za Hospitali ya Rufaa ya Sokoine na shilingi bilioni 1.26 zilitolewa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Fedha za ununuzi wa dawa kwa mwezi, ni wastani wa shilingi milioni 21,” alisema.

Ametoa kauli hiyo jana (Jumamosi, Oktoba 24, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Lindi na vitongoji vyake waliofurika kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika jana kwenye uwanja wa Ilulu mjini Lindi.

Akielezea kuhusu uboreshaji wa sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema katika Manispaa ya Lindi, kuna magari matano ya kubeba wagonjwa kwa ajili ya vituo vya afya Mjini, Mnazimmoja, Kitomanga, Milola na Rutamba.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko mkoani Lindi kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwanadi mgombea ubunge wa jimbo la Lindi, Bi. Hamida Abdallah na wagombea udiwani wa kata 20 za jimbo hilo.

Kuhusu sekta ya maji, alisema sh. bilioni 50 zimetolewa kwa ajili ya miradi mikubwa ya maji ikiwemo ujenzi wa skimu ya pampu Mtutu, skimu ya pampu Cheleweni, Narunyu, Tandangongoro na Muungano na kwamba zimesaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwenye mji wa Lindi.

“Fedha hizo zimetumika pia kwa ajili ya mradi wa maji safi na usafi wa mazingira Lindi Mjini (Mradi wa Maji Ng'apa) na kwenye mradi wa maji Ng'apa kijijini na usambazaji mtandao wa mabomba,” alisema.

Alisema sh. bilioni 1.26 zilitolewa kwa ajili ya miradi mingine ya maji ikiwemo ya kuchimba visima virefu katika maeneo ya Jangwani, Nanyanje, Kitumbikwela, Nachingwea, Kitunda, Likotwa, Mtange, Tulieni, Mitumbati, Mayani na Ngongo-Nanenane.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa alisema mkoa wa Lindi utanufaika zaidi kwa sababu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimeamua kuanzisha kitivo cha kilimo mkoani humo. “Taratibu zimeshakamilika na tumewapa ekari 150 katika eneo la Ngongo ili waweze kujenga kitivo cha kilimo,” alisema.

Leo Mheshimiwa Majaliwa anaendelea na kampeni kwenye jimbo la Liwale.

(mwisho)