MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuimarisha mfumo wa bima ya afya nchini ikiwemo mifuko ya bima za afya (NHIF na CHF) ili kufikia lengo la Serikali la kuwa na bima ya afya kwa wananchi wote, ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM.

Ilani ya uchaguzi inaelekeza Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo iendelee kutoa kipaumbele katika sekta ya afya kwa kuwa inagusa maisha ya Watanzania na ustawi wa Taifa huku lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya  bora ili waweze kushiriki katika shughulli za ujenzi wa Taifa na kuboresha maisha yao

Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Oktoba 10, 2020) alipozungumza na wananchi katika mikutano ya kampeni ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge jimbo la Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava na wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM, ambapo aliwaomba wananchi hao wawachague wagombea wa CCM ili waweze kushirikiana kuwaletea maendeleo.

Mheshimiwa Majaliwa alisema awali Serikali ilianzisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ambao ulihusisha watumishi wa umma na baada ya kupata mafanikio ilianzisha Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ambapo wananchi wanajipangia kiasi cha kuchangia katika maeneo na kuwawezesha kupata huduma za afya bure pamoja na familia zao.

“Awali mfuko huu wa CHF uliwezesha wananchi kutibiwa ndani ya wilaya zao tu ambapo kwa sasa umeboreshwa na kuwawezesha kutibiwa ndani ya mikoa yao. Baada ya kupata mafanikio makubwa katika uendeshaji wa mifuko kwa sasa Serikali inaandaa utaratibu wa kutoa huduma za afya kwa Watanzania wote na tayari kazi imeanza kwa muswada kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa alisema changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya katika halmashauri ya wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kuwa historia baada ya Serikali kutoa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Makuyuni, ambapo tayari ujenzi wa majengo sita umekamilika na jengo moja linamaliziwa.

Pia, Serikali imetoa shilingi milioni 598.6 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Mkumbara na shilingi milioni 200 kimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo kingine cha afya cha Kerenge, ambapo ujenzi wa vituo hivyo tayari umekamilika na taratibu za ununuzi wa vifaa tiba unaendelea kufanyika.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya hiyo, Mheshimiwa Majaliwa alisema

Serikali imetoa shilingi bilioni 3.188 kwa shule za msingi 138 kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa Maofisa Elimu Kata na Walimu Wakuu huku shilingi bilioni 2.50 zimetolewa kwa shule 28 za sekondari kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa Wakuu wa Shule.

“Shilingi bilioni 1.410 zimetolewa kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya madarasa, vyoo na ofisi kwa shule 58 ikiwemo ujenzi wa madarasa ya shule za msingi za Mruazi, Gereza, Kwamzindawa, Bombo Majimoto ,Mswaha, Lewa na Mkumbara na shilingi bilioni 1.568 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya madarasa, vyoo na maabara kwa shule za sekondari za Madago, Mkalamo, Mashindei, Mkomazi, Buiko, Patema, Kwagunda, Mazinde Day, Hale, Mnyuzi na Bungu.”