Kamati ya Maadili ya Kitaifa imemtaka Mgombea Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutofanya kampeni kwa muda wa siku saba kuanzia leo Oktoba 3 hadi Oktoba 9, 2020.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Kamati ya Maadili ya Kitaifa, Emmanuel Kawishe, amesema kuwa hatoruhusiwa kufanya kampeni zake wala kumnadi mgombea mwingine yeyote.


Kawishe amesema kuwa, “Adhabu inatakiwa kutekelezwa kwa kuwa imetolewa na chombo chenye mamlaka ya kisheria na kwa kuzingatia utaratibu, mgombea Urais wa Chadema anatakiwa kuheshimu na kutekeleza adhabu hiyo kama ilivyotolewa”.


Ameongeza kuwa, “Endapo mgombea huyo atadharau uamuzi wa kamati na kufanya kampeni atambue kuwa kamati imepewa mamlaka ya kuelekeza makosa mengine kwenye vyombo vingine kadri itakavyoona inafaa, suala la Tundu Lissu limetangazwa kwa sababu ni sehemu ya adhabu aliyopewa na kamati. 


Kamati sio Tume ya Taifa ya Uchaguzi bali ni chombo kinachoundwa na vyama vyote vyenye wagombea wa kiti cha Urais kikiwemo CHADEMA “, amesema Kawishe Katibu wa Kamati ya Maadili ya Kitaifa