BAADA ya kutua nchini Kocha Mkuu wa Yanga, Cedric Kaze ameanza kazi kwa kuzuia mechi za kirafiki ambazo timu hiyo ilikuwa icheze ili kuweza kumpa nafasi ya kukiangalia kikosi hicho na kukifanyia kazi.


 


Kaze ametua Yanga juzi Alhamisi akitokea Canada alipokuwa akiishi tayari kwa kuanza kazi ya kukinoa kikosi hicho baada ya kupokea kijiti kutoka kwa Kocha Mserbia, Zlatko Krmpotic aliyesitishiwa kibarua Oktoba 3.


 


Taarifa ambazo Championi Jumamosi imezipata kutoka ndani ya bechi la ufundi la Yanga zinasema kuwa, timu hiyo ilipanga kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya URA ya Uganda na Transit Camp lakini Kaze ameamua kuzizuia akitaka kukinoa zaidi kikosi chake.


 


“Awali tulikuwa na mechi mbili za kirafiki katikati ya wiki hii dhidi ya URA na Transit Camp lakini kocha Kaze amezizuia zisichezwe hadi atakapoamua, anataka kwanza akinoe kikosi kwa muda lengo ni kuhakikisha anashinda kila mchezo ligi itakapoanza,” alisema mtoa taarifa huyo.


 


Championi Jumamosi lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela kuzungumzia suala hilo alisema kuwa hayupo Dar hivyo hana la kusema kwa kuwa yuko nje ya timu.