VIONGOZI mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole na Mgombea Ubunge Viti Maalum Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile wamejitokeza katika kituo cha kupiga kura cha Kilimani jijini Dodoma kupiga kura ya kuchagua Rais, Mbunge na Diwani huku wakieleza kuridhishwa na muamko wa wananchi pamoja na hali ya amani na utulivu iliyopo.

Akizungumza baada ya kupiga kura Dk Bashiru amewataka watanzania kuzidi kujitokeza kwa wingi kwenye vituo walivyojiandikisha ili waweze kutimiza haki yao ya Msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka.


Kwa upande wake Polepole ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea wananchi na kuelekeza ili waweze kupiga kura bila usumbufu wowote.

" Nimeridhika na hali ya utulivu, wananchi wamehamasika sana na uchaguzi huu, niwaombe wanaokuja vituoni kupiga kura wakishamaliza warudi majumbani mwao wasubiri matokeo," Amesema Ditopile