Kamati ya Madili ya Kitaifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepigilia msumari wa mwisho kuwa adhabu iliyotolewa na kamati hiyo kwa mgombea Urais kwa tiketi ya CHADEMA Mhe.Tundu Lissu ni sahihi na haruhusi kupanda kwenye jukwaa lolote la siasa hadi adhabu hiyo iishe.

Katibu wa Kamati ya Maadili Kitaifa Emmanuel Kawishe akizungumza na vyombo vya habari juu ya suala la kufungiwa kwa siku saba kwa Tundu Lissu amesema mgombea huyo wa Urais hajaadhibiwa na Tume hiyo ya Uchaguzi bali ameadhibiwa na wenzake kutoka vyama 15.

Bwana Kawishe amesisitiza kwamba Endapo Mgombea huyo wa Urais Mhe.Tundu Lissu atayadharau maamuzi ya kamati hiyo na kufanya kampeni basi atambue kwamba kamati imepewa mamlaka ya kuelekeza makosa mengine kwenye vyombo vingine kadiri itakavyoona inafaa.

Kuhusu Lissu kupelekewa taarifa ya adhabu hiyo, Kawishe amesema “Tume haimpelekei taarifa mgombea mmoja mmoja, taarifa inapelekwa kwa makatibu wakuu wa vyama vyao, hivyo madai ya Tundu Lissu kuwa hajapokea taarifa ni uongo” -Amesema Kawishe.

Ameongeza kuwa suala la Lissu limetangazwa kwa sababu ni moja ya sehemu adhabu aliyopewa na kamati, hivyo atambue kwamba kamati sio tume ya uchaguzi bali ni chombo kinachoundwa na vyama vyote vyenye wagombea wa kiti cha Urais.

The post Kamati ya Maadili yasema adhabu aliyopewa Lissu ni sahihi appeared first on Bongo5.com.