KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUJERUHI

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia SALOME BUYA [23] Mkazi wa Mnazi kwa Ndomba wilayani Mbarali kwa tuhuma za kumjeruhi vibaya sehemu ya shingoni TABIA ABDALAH [38] Mkazi wa Msesule.


Tukio hili limetokea mnamo tarehe 06.10.2020 majira ya saa 18:00 jioni huko Kijiji cha Mnazi, Kata ya Imalilosongwe, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya ambapo mtuhumiwa SALOME BUYA alimjeruhi kwa kumchoma kisu sehemu ya shingoni upande wa kisogoni TABIA ABDALAH [38] Mkazi wa Msesule na kupelekea kupoteza fahamu.


Awali kabla ya tukio hilo, TABIA ABDALAH pamoja na wanawake wengine walimuita SALOME BUYA na kumtuhumu kuwatangazia wenzake kwa watu pindi wakichepuka nje ya ndoa zao. Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliozuka baina yao baada ya kutuhumiana kutoleana nje siri za ndoa. 


Aidha SALOME BUYA pia amepata majeraha kidogo sehemu ya puani. Majeruhi amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Mbarali kwa matibabu hali yake sio nzuri. Upelelezi wa shauri hili unaendelea.


KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA UNYANG’ANYI WA KUTUMIA NGUVU NA KUJERUHI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia MASUNGA YANORA @ PAULA [35], Mkazi wa Bariadi Mkoa wa Simiyu kwa tuhuma za kumvamia na kumjeruhi kwa kumpiga fimbo SIKUJUA MAYENGA [30] Mkazi wa Mpembe Pepea sehemu ya kichwani, kifuani na mbavu za kushoto. 


Ni kwamba mnamo tarehe 07.102020 majira ya saa 00:15 usiku huko Kitongoji cha Mpembe, Kijiji na Kata Lualaje, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. SIKUJUA MAYENGA alivamiwa nyumbani kwake na watu watatu ambao aliwafahamu kwa sura waliokuwa na fimbo na kumjeruhi kichwani, kifuani, mbavu za kushoto na baada ya tukio hilo watuhumiwa hao walitokomea kusikojulikana.


Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi lilifanya msako na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa MASUNGA YANORA @ PAULA [35]. Mtuhumiwa amehojiwa na amekiri kufanya tukio hilo huku akieleza kuwa lengo lilikuwa ni kumuua KIJA MALIMI mume wa SIKUJUA MAYENGA lakini baada ya kumkosa ndipo wakamshambulia mke wake. 


Mtuhumiwa anadai aliitwa na JUMA MASANJA, Mkazi wa Kijiji cha Lualaje Wilaya ya Chunya kuja Mpembe kutekeleza mauaji ya kumuua KIJA MALIMI kwa ujira wa Tshs 3,000,000/=. Chanzo cha tukio ni wivu wa kimapenzi ambapo JUMA MASANJA anamtuhumu KIJA MALIMI kuwa na mahusiano ya kimapenzi na mke wake. Upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na msako mkali dhidi ya watuhumiwa waliohusika kwenye tukio hili.


KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia SAMSON KYANDO [26] Mkazi wa Mswiswi Wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za mauaji ya mke wake aitwaye CECILIA WILSON [24] Mkazi wa Mswiswi.


Ni kwamba mnamo tarehe 04.10.2020 majira ya saa 20:00 usiku huko Kijiji cha Mswiswi mtuhumiwa alimshambulia CECILIA WILSON [24] kwa kumpiga fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia majeraha hali iliyopelekea kupelekwa Hospitali ya Misheni Chimala kwa matibabu.


Ambapo mnamo tarehe 06.10.2020 majira ya saa 04:00 usiku CECILIA WILSON [24] Mkazi wa Mswiswi alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini hapo. Chanzo cha tukio hilo ni ugomvi wa kifamilia baina ya marehemu na mtuhumiwa. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.


WITO WA KAMANDA:

Ninatoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake wajenge tabia ya kutafuta suluhu ya migogoro yao kwa kukaa meza moja ya mazungumzo au kuwashirikisha watu wa karibu ili kupata suluhisho la migogoro yao.

T

Aidha ninatoa rai jamii kukemea uhalifu na kutoa taarifa mapema za viashiria vya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa viongozi wao wa mitaa, kata au tarafa kwani ni walinzi wa amani katika maeneo yao kwa ajili yah atua zaidi za kisheria ikiwa ni pamoja na kukaa meza moja ili kutafuta suluhisho.  


                                                            Imetolewa na;


[ULRICH O. MATEI -SACP]


KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.