Onyo: Habari hii ina video ya kuogofya

Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Iraq na eneo la Uarabuni walipigwa na butwaa kufuatia habari za mwananke mmoja ambaye aliwarusha wanawae wawili katika daraja moja la mto Tigris katika mji mkuu wa Baghdad.


Kanda ya video iliosambaa katika mitandao ya kijamii, ilimuonesha mwanamke aliyembeba mtoto mmoja na kumshika mkono mwengine kabla ya kuwarusha mtoni bila huruma.


Kulingana na mtandao wa BBCArabic Siku mbili baadaye, polisi walitangaza siku ya Jumatatu jioni kwamba walipata mwili wa mtoto mmoja huku mwili wa ndugu yake ukiendelea kutafutwa.

Wanaharakati walisema kwamba watoto hao wawili ni watoto wa mwanamke huyo wa Iraq , wakidai kwamba aliamua kuwatosa majini kutokana na hali mbaya ya kiuchumi nchini humo.


Wakati huohuo vyanzo vya habari vilidai kulikuwa na migogoro ya kinyumbani kati ya mwanamke huyo na mumewe wa zamani aliyeshinda kesi ya kuishi na watoto hao.


Vilevile wanaharakati walisambaza video waliosema ilikuwa ile ya baba ya watoto hao wawili ambaye alikuwa karibu na eneo la tukio hilo , kulingana na kile ambacho wanaharakati wanasema.


Kanda ya video ilimuonesha baba huyo akiwalilia watoto wake wawili.


Tukio hilo liliwashtua raia wengi wa Iraq na kuvutia vyombo vya habari pamoja na wanablogu katika mataifa mengi ya Uarabuni.


Watangazaji walishutumu kitendo hicho , walichokitaja kuwa cha unyama na kutaka mwanamke huyo apewe adhabu kali.


Wengine walihoji sababu ya kitendo hicho na hukumu ya kitendo kama hicho.


Wengine pia walitaka kufanyiwa mabadiliko kwa sheria za kuchukua na kuishi na watoto pamoja na zile za kuwalinda watoto.


Wanaharakati na wataalamu waliokutana mbele ya eneo la tukio hilo walishindwa kuelewa fikra za mwanamke huyo na jinsi alivyochagua njia ya kuwauawa watoto hao badala ya kuwapeana kwa mumewe wa zamani.


Hivyobasi wengi wao walitaka kuwepo kwa subra hadi matokeo ya uchunguzi yatakapotolewa na wakataka utafiti kufanywa kuhusu ongezeko la uhalifu badala ya kuwekwa kwa hukumu kali.


Wanaharakati hao vilevile waliitaka serikali kubaini sababu zinazoathiri akili za wazazi na kubuni vitengo vya kushughulikia kesi za kuishi na watoto, suala ambalo humaliza migogoro kati ya pande mbili ambapo watoto ndio waathiriwa.


Pia wanaamini kwamba kukabiliana na umasikini na ujinga mbali na kuwapatia haki wanawake waliopewa talaka kutapunguza uhalifu kama huo.


Upande mwengine, wengine walisema kwamba umasikini na dhiki haufai kumfanya mtu kutekeleza uhalifu kama huo ambao unaonesha wazi kwamba mtu hana utu.