Na. Lilian Shembilu-MAELEZO
Katika kutekeleza majukumu yake kuelekea siku ya Uchaguzi Mkuu 2020, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ina wajibu wa kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Uchaguzi,  Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Sheria hii inataja wajibu wa NEC kuwa ni kuratibu uandikishaji wa wapiga kura, kuhuisha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kusimamia zoezi zima la uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivi karibuni NEC ilikabidhi kwa Vyama vya Siasa nakala tepe ya Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo litakuwa na majina, picha na taarifa za mpiga kura ambazo zinawasaidia wasimamizi wa uchaguzi kugundua wapiga kura wanaongia kituoni kwa ajili ya kupiga kura kwa kuhakikisha maelezo na picha yaliyopo kwenye kadi ya kupigia kura yanaendana na yale yaliopo katika daftari ikiwa ni sehemu muhimu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba, 2020

Hilo limefanyika kwa mujibu wa kanuni ya 37 ya kanuni za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za mwaka 2018 ambayo inaelekeza Tume kuvipatia vyama vya siasa nakala ya daftari kwa ajili ya kuwatambua wapiga kura wanaoingia katika kituo cha kupigia kura ili kuweza kuwagundua wapiga kura hewa na wale ambao hawakujiandikisha.

Pamoja na maelekezo hayo ya Tume, kuna mambo muhimu ya kuzingatia siku ya kupiga kura. Mpiga kura anatakiwa kufahamu kituo chake cha kupigia kura, ambacho ni pale alipojiandikisha au alipoboresha taarifa zake na muda wa kupiga kura.

Siku ya uchaguzi vituo vya kupigia kura hufunguliwa saa moja kamili, asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni kwa upande wa Tanzania Bara na upande wa Zanzibar vituo hufunguliwa saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja kamili jioni.

Kituo cha kupigia kura hubandikwa bango jeupe lililoandikwa KITUO CHA KUPIGIA KURA na nje ya kituo hubandikwa mabango yanayotoa Elimu ya Mpiga kura likiwepo bango la Tahadhari na mchakato kituoni. Hii itapelekea mpiga kura yoyote kuwa na uhakika na kituo cha kupigia kura.

Siku ya kupiga kura, kila mpiga kura anatakiwa kufika kituoni katika muda uliotangazwa na NEC ambao ni kuanzia saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni. Muda huo uliopangwa na Tume ukiisha hakuna mtu mwingine yeyote atakaye ruhusiwa kupiga kura. Inapofika saa kumi kamili mlinzi wa kituo atakaa nyuma ya mtu wa mwisho ili watu wote walio mbele ya mlinzi huyo waweze kupiga kura.

Aidha, NEC inashauri kila mpiga kura kutunza kadi yake na kuitumia kupigia kura siku hiyo na si vinginevyo.  Katika kuhakikisha kuwa kila raia aliyejiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura anatumia haki yake ya kuchagua viongozi anaowapenda, NEC imetoa nafasi ya mpiga kura kutumia kitambulisho mbadala endapo atakuwa amepoteza au kuharibu kadi yake ya kupiga kura. Mpiga kura anaruhusiwa kutumia Kitambulisho cha Taifa, Pasi ya kusafiria au Leseni ya udereva ambavyo havijaisha muda wake lakini pia awe kwenye kituo alichojiandikisha tu, kwa masharti kuwa majina yake yafanane na yale yaliyopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura.

Pamoja na kwamba kila mpiga kura anakuwa na maamuzi ya kuwa katika chama chochote cha siasa akipendacho siku ya uchaguzi mpiga kura hatakiwi kuvaa nguo zinazoashiria itikadi ya chama fulani cha siasa.

Siku ya kupiga kura kuna makundi maalumu ambayo yatapewa kipaumbele, NEC imeyaainisha makundi hayo kuwa ni mama wajawazito, wakina mama wenye watoto wachanga waliofika nao vituoni, wazee, wagonjwa na watu wenye mahitaji maalumu kama vile walemavu wa viungo, wasiosikia na wasioona

Ikiwa jina la mpiga kura halitaonekana katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura kituoni mhusika anatakiwa amuone Karani Mwongozaji wa wapiga kura (Direction Clerk) ambaye atamsaidia kupata maelekezo au kumuonesha kituo chake cha kupigia kura.

Lakini pia kila mpiga kura anatakiwa kufahamu kuwa  vituo vya kupigia kura ni vile vilivyotumika wakati wa kuandikisha wapiga kura mwaka 2015 na pia wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2019 na 2020 ambavyo vitakuwa kwenye mitaa, vitongoji na vijiji katika kata zote za Mikoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mahali pa kupigia kura ndio mahali hapo tu ambapo jina lako litaonekana ndipo utaweza kupiga kura. Siku hiyo ya kupiga kura ikiwa jina lako halionekani katika orodha iliyopo kituoni basi  huenda umekwenda katika kituo ambacho si chako na hii ndio sababu Tume hubandika orodha ya wapiga kura kituoni siku 8 kabla ya uchaguzi ili uweze kujua kilipo kituo chako.

Mpiga kura anaweza kuhakiki taarifa zake kwa njia ya simu yako ya mkononi kujua kituo chake kwa kupiga simu kwenda namba *152*00# kisha kufuata maelekezo au anaweza kupiga simu namba 0800112100 na huduma hizi ni bure.

Aidha, makarani waongozaji wapiga kura watakuwepo katika vituo vya kupigia kura siku ya uchaguzi kuwasaidia wapiga kura kutambua vituo vyao hivyo mpiga kura yeyote ambaye ana tatizo anatakiwa kuuliza makarani watakaowakuta ili waweze kupata ufumbuzi wa maswali watakayokuwa nayo.

Pamoja na mambo mengi ambayo Tume ya Uchaguzi imekuwa ikiwasisitiza wapiga kura wote na kutoa elimu, kuratibu na kusimamia watu wanaotoa elimu ya uchaguzi kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kila Mpiga kura anapaswa kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa kuepuka matatizo yoyote ambayo yanaweza kujitokeza kwenye Kituo cha Kupigia kura na kusababisha kukosa haki ya msingi ya kupiga kura.

Wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika zoezi la kupiga kura bila kuwa na wasiwasi wala hofu kwani, upigaji kura upo kisheria, chini ya kanuni ya 3.1 (b) ya maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015. Serikali imepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa kunakuwapo hali ya usalama, amani na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi na baada ya uchaguzi.

MWISHO