Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa hospitalini tangu Ijumaa baada ya kugunduliwa kuwa na ugonjwa wa COVID-19. Madaktari wake wameridhika na maendeleo ya matibabu yake.

Waandishi habari ambao kwa kawaida huongozana na rais, hata hivyo, wamesema kwamba katika saa 24 zilizopita hali ya kiafya ya rais huyo ilikuwa ni ya wasiwasi wakinukuu chanzo cha kuaminika.

Katika video inayomuonesha akiwa hospitalini, Trump amesema kwamba awali kweli alikuwa akijisikia vibaya wakati alipopelekwa hospitali, lakini sasa hivi anaendelea vizuri.

Aidha rais huyo alitetea uamuzi wake wa kuendelea na mikutano yake ya kampeni ya watu wengi licha ya kitisho cha janga la virusi vya corona. Trump alisema hakuwa na jinsi, kama kiongozi alilazimika kukabiliana na changamoto hiyo kwani hakuwa tayari kujifungia ndani wakati wote.

Mke wa rais Melania Trump, ambaye pia amethibitishwa kuapata maambukizi ya Covid-19, pia nae “anaendelea vizuri”, amesema Daktari wake binafsi Sean Conley.

Orodha ya watu wengine ambao wamethibitishwa kupata maambukizi walio karibu na Bwana Trump ni pamoja na msaidizi wake Hope Hicks – anayeaminika kuwa wa kwanza kuonesha dalili – mkuu wa timu ya kampeni Bill Stepien na aliyekuwa mshauri wa Ikulu Kellyanne Conway. Maseneta wa Republican Mike Lee na Thom Tillis pia nao wamesemakana kupata maambukizi.

The post Daktari athibitisha afya ya Trump inaendelea vizuri appeared first on Bongo5.com.